Yanga Hawazuiliki, Waonyesha Dalili 5 za Ubingwa





YANGA huu msimu ni wao, kutwaa kombe la Ligi Kuu Bara wana asilimia kubwa sana, kwani wameonyesha dalili zote za kuchukua ubingwa huo waliokosa kwa misimu minne mfululizo.

 

Yanga hadi sasa wanaongoza kila kitu dhidi ya timu zote zinazoshiriki ligi kuu, hiyo ikiwa ni sababu ya kwanza. Wakiwa wamecheza mechi 13 sawa na dakika 1,170 bila kupoteza. Ni timu pekee ambayo haijapoteza mechi.

 

Sababu ya pili, Yanga wamekuwa wakipata alama kwenye kila uwanja, hasa vile viwanja vigumu ambavyo ni nadra kupata ushindi kwao.

Wakipata ushindi wa 2-0 dhidi ya Mbeya Kwanza, Uwanja wa Sokoine, wakiwachapa Coastal Union 2-0 pale Mkwakwani, wakiwaburuza Polisi Tanzania kwa mara ya kwanza wakiwa kwao kwa bao 1-0.

 

Wakiwachapa Tanzania Prisons kwa mabao 2-1, wakiwa kwao Uwanja wa Nelson Mandela. Uwanja pekee ambao bado umekuwa mgumu kwao ni ule wa Namungo wakitoka sare ya 1-1 kama ambavyo imekuwa kwa misimu yote.

Sababu ya tatu, Yanga wana wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao msimu huu kama ambavyo ilikuwa kwa Simba msimu uliopita. Fiston Mayele ameshafunga mabao saba.

 

Feisal Salum amefunga manne sawa na Saidoo Ntibazonkiza, Jesus Moloko amefunga mabao matatu, Khalid Aucho kafunga mawili na Dickson Ambundo, Djuma Shaban na Mukoko Tonombe ambaye kasepa, wamefunga moja moja.

Sababu ya nne, Yanga tayari amevuna alama nne dhidi ya timu ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, waliwachapa Azam FC 2-0 na kutoka suluhu na Simba.

 

Simba wameachwa na Yanga kwa pointi 10 hadi sasa na Azam wamepitwa pointi 14, hali ambayo inazidi kuwapa nafasi kubwa ya kuweza kutwaa ubingwa wa msimu huu.

Sababu ya tano, ari na morali ya wachezaji msimu huu na hiyo imesemwa na msemaji wa timu hiyo, Haji Manara, ambaye amesema kila mchezaji wa timu hiyo ananukia ubingwa.

 

Manara alisema: “Ukipita kwenye kambi ya Yanga kila mchezaji anazungumzia ubingwa, hakuna mchezaji ambaye hataki kuwa bingwa au kuwapa ubingwa Yanga msimu huu.

“Ubingwa ni wa Yanga, kama Yanga hatakuwa bingwa mimi nitahama nchi hii. Tuna kila nafasi ya kuchukua ubingwa huu.”

 

Kwa sasa Yanga wapo jijini Mwanza na kesho Jumamosi watacheza mechi ya mashindano ya Azam Sports Federation Cup dhidi ya Mbao FC. Mechi ikichezwa Uwanja wa CCM Kirumba.

ISSA LIPONDA, Dar es Salaam

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad