Yanga hii raha nyie, yani anatoka mtu wa maana, anaingia mtu mwenye balaa. Hilo limejidhirisha juzi Ijumaa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji ambapo ilishuhudiwa Yanga ikifanikiwa kuwatumia mastaa wake kuiangamiza vibaya timu hiyo kwa mabao 4-0 ndani ya
Uwanja wa Mkapa, Dar.
Ukiachana na ushindi huo, furaha kubwa kwa mashabiki wa Yanga ni pale ambapo benchi la ufundi la timu hiyo
lilipokuwa linafanya mabadiliko ambayo yalipelekea shangwe kubwa kwa mashabiki wa timu hiyo kuonesha kuukubali mziki wa timu yao.
Katika mabadiliko ambayo yaliibua shangwe kubwa kwa mashabiki wa Yanga ni pale ambapo alitolewa kiungo,
Khalid Aucho ambaye alifunga bao la nne, kisha akaingia Salum Abubakar ‘Sure Boy’, hili ni ingizo jipya kikosini hapo.
Shangwe lingine lilitokea wakati Fiston Mayele ambaye alikuwa mfungaji wa bao la kwanza katika mchezo huo aliyempisha Heriter Makambo.
Mbali na mabadiliko hayo, pia Yanga ilimtoa Feisal Salum na kuingia Mukoko Tonombe, Saido Ntibazonkiza alimpisha Deus Kaseke na Jesus Moloko nafasi yake ilichukuliwa na Farid Mussa.
Mbali na kufanyika kwa mabadiliko hayo, pia Yanga katika mchezo huo iliingia huku ikiwa imewakosa baadhi ya mastaa wake ambao wamekuwa katika sehemu ya kikosi cha kwanza msimu huu ambao ni Djuma Shabani, Kibwana Shomari ambao wote wanacheza beki wa kulia.
Wawili hawa ni majeruhi, huku Kipa namba moja, Djigui Diarra akienda kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Mali.
Katika kuonesha kuwa Yanga wana kikosi kipana na chenye ushindani, Benchi la Ufundi chini ya Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, waliamua kumtumia Dickson Job kucheza beki wa kulia ambaye kiuhalisia ni beki wa kati.
Furaha inakuja zaidi kwa mashabiki wa Yanga pale ambapo wakifikiria majembe yao mapya ambayo bado hayajacheza itakuwaje endapo yatakuwa tayari kwa ajili ya kuanza kuitumikia timu hiyo.
Yanga katika wachezaji wao wapya tayari imewatumia golikipa Aboutwaleeb Mshery na Sure Boy, huku wengine akiwemo Denis Nkane na Chiko Ushindi wakiwa bado hawajaanza kazi.
Ni wazi sasa Yanga inaweza kucheza mechi tofauti na vikosi vikosi viwili na bado ikafanya vizuri kwa namna ambavyo Nabi anavyoijenga timu isiyofungika kwani mpaka sasa imecheza mechi 11 za Ligi Kuu Bara na kushinda
tisa, sare mbili.
Haijapoteza ikiongoza ligi kwa pointi 29. Spoti Xtra tumekuchambulia vikosi viwili hatari vya Yanga ambavyo kama timu pinzani ikienda kizembe, itachakazwa.
Kikosi cha kwanza; Djigui Diarra, Djuma Shabani, Yassin Mustapha, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Yanick Bangala, Jesus Moloko, Khalid Aucho, Fiston Mayele, Feisal Salum na Saidi Ntibazonkiza.
Kwa upande wa kikosi cha pili, kipo hivi; Aboutwaleeb Mshery, Kibwana Shomary, David Bryson, Mukoko Tonombe, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Zawadi Mauya, Denis Nkane, Salum Aboubakar, Heriter Makambo, Farid Mussa na Chiko Ushindi.
Wachezaji wengine ambao hapo hawajaingia kwenye kikosi chochote ni kipa Erick Johora, beki wa kulia, Paul Godfrey, kiungo Deus Kaseke na washambuliaji Yusuph Athuman na Yacouba Songne ambaye kwa sasa ni majeruhi.