ACT ‘yanunua’ kesi makada wa CHADEMA waliofungwa



CHAMA cha ACT-Wazalendo mkoani Lindi, kinajipanga kukata rufani kupinga adhabu ya kifungo waliyopewa wanachama wanne wa CHADEMA Kata ya Majengo, Halmashauri ya Mtama, kwa makosa mbalimbali likiwamo la kuharibu mali wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Tamko la kusudio hilo lilisomwa na Mwenyekiti wa ACT wa Mkoa huo, Rashidi Mchinjita, alipokuwa anatoa taarifa fupi ya hali ya kisiasa mkoani Lindi katika mkutano wa kumtambulisha kwa viongozi na wanachama wa ACT Mwenyekiti wa Taifa, Duni Juma Haji.

Wafuasi hao waliofungwa miaka nane kila mmoja ni Diwani aliyeshindwa uchaguzi mwaka 2020, Rajabu Hassani Mfaume, kampeni meneja wake, Dadi Hassani Shayo, Hamisi Abdallah Malege na Moshi Hamisi Mbelenye.

Mchinjita akiwasilisha taarifa kwenye mkutano huo uliojumuisha viongozi na wanachama kutoka wilaya nne kati ya tano za Mkoa wa Lindi, alisema kufuatia hukumu waliyopewa wafuasi wa Chadema, wanajiandaa kukata rufani.

“Tutakwenda gerezani ili kuzungumza nao ili kushauriana na kufahamu mawakili waliokuwa wanawatetea tuweze kukata rufani,” alisema Mchinjita.


 
Alisema pia watapenda kufahamu mawakili hao maeneo yepi walikwama kuwanusuru wateja wao.

Mwenyekiti huyo alisema pamoja na changamoto zilizopo, zikiwamo za kiuchumi, lakini kufuatia udugu wao na wana CHADEMA wa kuzaliwa na wa kisiasa, wanalazimika kuingilia kati kukata rufani kwa ajili ya kuwanusuru na adhabu waliyopewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mkoa wa Lindi wiki iliyopita.

Februari 18 mwaka huu, Mahakama hiyo iliwahukumu makada hao wa CHADEMA kutumikia kifungo cha miaka minane kila mmoja, baada ya kupatikana na hatia ya makosa mbalimbali, likiwamo kuharibu mali za umma na binafsi.


Mali zilizoharibiwa kwa kuchomwa moto ni Ofisi ya Serikali Kata ya Majengo na pikipiki moja iliyokuwa inamilikiwa na mtu binafsi na kujeruhi watu watatu akiwamo Askari Polisi WP 7657 Esther Kalaminyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad