Adebayor kuvunjiwa benki Simba, waifuata Berkane



BAADA ya kulazimisha sare ugenini juzi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, jana saa 12:00 jioni kwa saa za Niger ambazo ni sawa na saa 2:00 usiku kwa Afrika Mashariki, wawakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa ngazi ya klabu, Simba walikwea pipa juu kwa juu ....

juu kuelekea nchini Morocco tayari kwa mchezo unaofuata dhidi ya RS Berkane.

Simba juzi iliondoka na pointi moja baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Union Sportive Gendarmerie Nationale (USGN) hiyo ikiwa mechi yake ya pili na ya kwanza ugenini kwenye hatua ya makundi, hivyo kukaa kileleni mwa Kundi D ikiwa na alama nne kutokana na kushinda 3-1 katika mechi ya kwanza nyumbani dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast ambayo juzi nayo ilitoa kipigo kama hicho ikiwa kwao dhidi ya RS Berkane.

Katika mchezo wa juzi, winga wa Union Sportive Gendarmerie Nationale, Victorien Adebayor, ambaye alionyesha kiwango cha hali ya juu alihusishwa na kutua Msimbazi msimu ujao, mwenyewe akisema hawezi kukataa ofa hiyo kama itakuja.

Winga huyo raia wa Niger, alionyesha uwezo mkubwa kwenye mechi hiyo, akiwachachafya mabeki wa Simba, lakini alifunga mabao mawili katika mechi ya kwanza dhidi ya RS Berkane wakati wakipoteza kwa mabao 5-3.


 
"Simba ni timu kubwa Afrika na kila mara inafanya vizuri, ni fahari kuchezea timu kubwa kama hii, wachezaji wengi wangetamani kuichezea, hata mimi, ikitokea fursa siwezi kuiacha kama watanihitaji," alisema Adebayor alipohojiwa baada ya mechi hiyo kumalizika.

Alipoulizwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again', mapokeo yake kuhusu kauli ya winga huyo, alisema atamshawishi Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed "Mo" Dewji 'kuvunja benki' ili kumsajili Adebayor ambaye anaichezea USGN kwa mkopo.

"Nimemwona, ni mchezaji mzuri, nilishawahi kuongea na wakala wake huko nyuma, kwa bahati mbaya kwa sasa amesajiliwa nchini Denmark, hapa anacheza kwa mkopo. Lakini leo nimezungumza tena na wakala wake asubuhi na hata saa hizi mechi imeisha nimeongea naye tena, na nitaongea na rais wa klabu hii avunje benki kwa ajili ya kumpata mchezaji huyu asirudi Ulaya, kwa sababu ana uwezo mkubwa, ana nguvu na spidi na anajua kufunga. Huyu ni mchezaji wa kuichezea Simba, wala hawezi kurudi Ulaya," alisema Try Again.


Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco, ameeleza kuridhishwa na sare iliyopatikana ugenini juzi, huku akidai imepatikana kwenye mazingira magumu kutokana na baadhi ya wachezaji wake kukabiliwa na changamoto za kiafya zilizochangiwa na hali ya hewa.

"Tulitaka kushinda mechi hii, kwa sababu ndiyo malengo yetu, lakini ilishindikana kwa sababu nyingi, kwanza ugumu wa usafiri, hatukuwa na muda wa kujiandaa, tuliangalia mikanda ya mechi zao haraka haraka na wala hatukuwa na muda wa kufanyia mazoezi uwanjani, badala yake tuliwaelekeza tu wachezaji jinsi gani ya kufanya. Nashukuru wachezaji wetu walifuata maelekezo. Kupata sare ugenini kwa hali kama hii ni jambo la kujivunia kwa sababu pia hali ya hewa ya joto na vumbi lilituathiri wakati wa mchezo, kupumua kwa wachezaji ilikuwa shida pia," alisema kocha huyo.

Yalikuwa ni mabao ya Wilfried Gbeuli dakika ya 12 na Bernard Morrison dakika ya 84 yaliyoifanya mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya makundi kuisha kwa sare ya bao 1-1.

Katika hatua nyingine Meneja Habari wa Simba, Ahmed Ally, amesema kikosi hicho kilitarajiwa kuondoka jana saa 12:00 jioni kwa saa za Niger sawa na saa 2:00 usiku kwa Tanzania, ambapo kitapitia Uturuki kabla ya kutua Morocco tayari kwa mechi yao dhidi ya RS Berkane itakayopigwa Jumapili wiki hii.


 
Alisema wamelazimika kwenda mapema nchini humo kutokana na hali ya baridi kali iliyoko huko kwa sasa, hivyo kuwapa muda wachezaji wakuizoea na kupumzika ambapo wataweka kambi ya siku tano jijini Casablaca kabla ya kuielekea mjini Berkane kwa mchezo huo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad