Meneja wa Habari na Mawasilino wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Ahmed Ally, ameonesha matumaini na imani kwa kikosi cha klabu hiyo kulipa cha kufungwa na RS Berkane katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika Jana Jumapili (Februari 27).
Simba SC ilipoteza mchezo huo wa ‘Kundi D’ kwa mabao 2-0, ikiwa ugenini nchini Morocco na kushuka kileleni mwa msimamo wa Kundi hilo hadi nafasi ya pili kwa kusaliwa na alama 04.
Ahmed Ally ameonesha imani na matumaini hayo kupitia andiko alilolichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo mwisho amemalizia na neno MSIHOFU WALA MSIHUZUNIKE.
Ahmed Ally ameandika: Tunarudi kwetu sasa…. Nyumbani kwetu na sisi… Kwenye ufalme wetu
Save the date MARCH 13 2022,
Siku ambayo Rs Barkane watavuta pumzi ya moto, siku ambayo Barkane wataiona Simba halisi
Wana Simba wenzangu tujiandae kwa siku hii ya kihistoria, hizi ndio mechi zetu za kujidai
Hatuna tunachohitaji siku hiyo zaidi ya Alama TATU na Insh Allah kwa heshima ya Nchi zitapatikana.
MSIHOFU WALA MSIHUZUNIKE
Simba SC itakua mwenyeji wa RS Berkane katika mchezo wa Mzunguuko wa nne wa ‘Kundi D’ Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Machi 13.
Wakati Simba SC ikishuka hadi nafasi ya pili katika Msimamo wa ‘Kundi D’ kwa kuendelea kuwa na alama 04, RS Berkane wamekwea hadi kileleni kwa kufikisha alama 06, huku USGN iliyoichana ASEC Mimosas mabao 2-0 jana Jumapili (Februari 27) ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama nne.
ASEC Mimosas inaburuza mkia wa kundi hilo kwa kuendelea kuwa na alama 03.