WAKATI watu duniani wakiadhimisha Siku ya Wapendanao jana Jumatatu, tarehe 14 Februari 2022, Wille Mwakapimba mkazi wa Mpanda Hotel mjini Mpanda mkoani Katavi alikutwa amejinyonga kwa kamba chumbani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Katavi … (endelea).
Kabla ya kujinyonga inadaiwa aliacha barua yenye ujumbe alisikia ujumbe wa sauti ya marehemu mama yake, ikimtaka aende kaburini akafukue kaburi lake kwenye makaburi ya Mwangaza, kwamba kuna vitu vya kishirikina vimefukiwa kwenye kaburi hilo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kivuko Koni, kata ya Shanwe, Michael Sikenyenzi alisema tukio hilo, lilitokea jana Jumatatu saa nne na robo kwenye kata ya Shanwe, Mpanda, muda mfupi baada ya kutoka kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mpanda.
Alisema taarifa ya tukio hilo aliipata baada ya kupigiwa simu ikimtaka aende nyumbani kwa Hawa kuliko na tukio la mtu kujinyonga.
Alibainisha baada ya kufika nyumbani kwa Hawa, alikuta Mwakapimba amejinyonga chumbani, hivyo kutoa taarifa Polisi, na askari kulifika eneo hilo.
Sikenyenzi alisema kwenye chumba hicho walikuta ujumbe wa maandishi ukieleza kuwa alisikia sauti ya marehemu mama yake ikimtaka aende kwenye kaburi la mama yake akafukue kuna vitu vimefukiwa na ndugu yake, ambaye amekuwa akiwafanyia ushirikina.
Alisema baada ya kusoma hiyo barua, walihoji ndugu wa marehemu waliofika eneo hilo akiwamo kaka yake mkubwa, aliyedai kuwa ni kweli, alikwenda makaburi ya Mwangaza.
Alifukua kaburi na kukuta kichwa kinachosadikiwa kuwa cha binadamu na sehemu za siri za mwanamke, sanda na kitambaa chekundu, na kuvichukua hadi dukani kwa ndugu yake aliyekuwa akimtuhumu kuwa ni mshirikina.
Alieleza baada ya kuvipeleka vitu hivyo tarehe 11 Februari 2022, kwenye duka hilo lililopo mtaa wa Mpanda Hotel, polisi walipata taarifa na kwenda kumkamata na kumweka mahabusu hadi kesho yake mchana.
Alifafanua, kuwa kabla hajajinyonga alitoka kituo cha Polisi alikokwenda kuripoti kama alivyotakiwa na Jeshi hilo.
Mkewe, Hawa Ayub alisema yeye na marehemu walikuwa wakiishi kama mume na mke kwenye nyumba aliyoachiwa na mumewe wa kwanza aliyefariki dunia. Alisema yeye na Mwakapimba walijaaliwa mtoto wa kike.
Alisema alipigiwa simu na Mwakapimba akimtaka arudi nyumbani mapema kwani alikuwa na shida naye,
Alipofika nyumbani na kuingia chumba cha kulala akamwona mumewe tayari amejinyonga ananing’inia kwenye dari akiwa ametumia kamba na pembeni kukiwa na kigoda jirani na kitanda.
Mmoja wa majirani zao, Anastazia John alisema walisikia mayowe ya Hawa akiomba msaada na kufika eneo hilo na kushuhudia mwili wa marehemu ukining’inia.