Bunge lang’aka kukatika umeme mara kwa mara



By Sharon Sauwa
Dodoma. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imesema kukatika umeme mara kwa mara ni linaloweza kuzuilika endapo Serikali ingechukua hatua madhubuti kwa kutekeleza mpango wa ukarabati wa miundombinu ya Tanesco na kuipatia fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dustan Kitandula leo Februari 15, 2022 wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa Januari mwaka 2021 hadi Februari 2022.

Kitandula amesema wakati kamati ilipopokea taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini, ilielezwa sababu nyingi zikiwemo kutokuwa na matengenezo ya kutosha kwenye miundombinu ya ufuaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.

Ametaja sababu nyingine ni uchakavu wa miundombinu ya kufua, kusafirisha na kusambaza umeme, kuzidiwa kwa vituo vya kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na kuongezeka kwa watumiaji ukilinganisha na miundombinu iliyopo.


 
Amesema kamati Ilielezwa kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo, tayari Tanesco imeandaa mikakati mbalimbali ikiwemo ya muda mfupi, wa kati na mrefu na ili iweze kutekelezwa kikamilifu zinahitajika takribani Sh2 trilioni.

“Kamati inasikitishwa na sababu zilizotolewa kuhusu kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini, kwani ni jambo linaloweza kuzuilika endapo Serikali ingechukua hatua madhubuti kwa kutekeleza mpango wa ukarabati wa miundombinu ya Tanesco na kuipatia fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati,” amesema.

Kitandula amesema kutokana changamoto hizo Tanesco ipewe fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu katika mwaka huu wa fedha ili iweze kufanya ukarabati mkubwa wa miundombinu yake na kuondoa tatizo la kukatika umeme mara kwa mara.


“Tanesco iongezewe bajeti kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya ufuaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme ili iweze kukarabati miundombinu hiyo na kuondoa tatizo la umeme kukatika mara kwa mara,” amesema.

Amesema kutokana na kuongezeka kwa watumiaji wa umeme nchini Tanesco ifunge vifaa vyenye uwezo wa kusambaza umeme kwa wateja wengi ikiwemo kufunga mashine umba zenye uwezo wa kuhudumia wateja kadrii ya mahitaji yao.

Kitandula amesema ni muhimu bei ya umeme iangaliwe ili iwe huduma yenye kuleta ahueni kwa wananchi na kuangalia ubora na uhakika wa umeme wake  ili wateja wengi waweze kutumia hususan Viwanda vikubwa na ikibidi wawe na laini zao mahsusi ili shirika hilo iweze kupata mapato ya kutosha.

Ametaka pia wizara iwe inafanya tathmini ya hasara za kiuchumi ambazo nchi inapata kutokana na kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini na kuchukua hatua stahiki kama Kamati ilivyooelekeza ili kuepuka athari za kiuchumi ambazo nchi inazipata.

Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kujua athari za uchumi kwa nchi na Tanesco kuondokana na utendaji wa mazoea.

Kitandula amesema ipo haja kwa Serikali kufanya tathmini ya kina kuhusu gharama kubwa inazozitumia Tanesco katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.

Amesema matokeo ya thathmini hiyo yatumike kuijengea shirika uwezo kifedha ili hatimaye iweze kutekeleza majukumu yake kwa wakati.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad