KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeitaka Serikali ichunguze sababu za kutofautiana kwa mahitaji ya kiasi cha mishahara, katika baadhi ya halmashauri nchini, ili kudhibiti mishahara hewa serikalini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Wito huo ulitolewa juzi tarehe 17 Februari, 2022 kupitia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa LAAC, Grace Tendega, kuhusu uchambuzi wa kamati hiyo juu ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kwa hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2020.
“Kwa kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ndiyo zenye kanzi data ya Idadi halisi ya watumishi waliopo katika maeneo yao na kwa kuwa imebainika sasa kiasi cha mishahara kinachotolewa na Hazina, katika baadhi ya halmashauri ni kikubwa kuliko mahitaji halisi ya halmashauri zenyewe,” ilisema taarifa ya LAAC.
Taarifa hiyo ilisema “Serikali ichunguze sababu za kutofautiana kwa mahitaji ya kiasi cha mishahara, kati ya halmashauri za mkoa wa Tabora na Wizara ya Fedha (Hazina), kwa namna ilivyoelezwa katika Sehemu ya pili ya taarifa hii. Kisha kuchukua hatua kwa muijibu wa sheria kutokana na upotevu wa mishahara hiyo.”
LAAC iliishauri Serikali ihuishe mfumo wa mishahara unaotumiwa na Hazina na Mamlaka za Serikali za Mitaa, ili kupata kiasi sahihi cha mishahara inayopaswa kulipwa.
“Pendekezo hili linakusudia kudhibiti kuibuka upya kwa hoja ya mishahara hewa Serikalini na kuleta hasara bila sababu za msingi,” ilisema taarifa ya LAAC.
LAAC ilitoa wito huo, baada ya uchambuzi wake kuhusu taarifa ya ukaguzi wa CAG, kwa Serikali za Mitaa, kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni 2020, kubaini kuna kutofautiana kwa mahitaji halisi ya mishahara kwenye mfumo wa Hazina.
“Hoja hii ina viashiria vya kuibuka tena kwa mishahara hewa serikalini, kuna ushahidi kwamba kiasi cha mishahara kinachotolewa na hazina huwa ni kikubwa kuliko, kile kinachotakiwa katika Halmashauri,” ilisema taarifa ya kamati hiyo.
Taarifa ya LAAC ilitaja halmashauri zilizopokea fedha nyingi za mshahara kutoka Hazina ikilimnganishwa na kiwango kinachotakiwa ni, Halmashauri za Wilaya za Mkoa wa Tabora, Urambo, Kaliua na Uyui.
Taarifa hiyo ilionesha, Halmashauri ya Wilaya ya Urambo, mahitaji ya mshahara ilikuwa ni Sh. 13,162,727,251, lakini Hazina ilitoa Tsh. 13,308,458,790, hivyo kusababisha ziada ya Sh. 145, 731, 539.
“Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua, mahitaji ya Lawson yalikuwa ni Sh. 17,679,189,899, lakini Hazina ilipeleka Tsh. 17,889,094,180, hivyo kuwa na ziada ya Sh. 209,902,281,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza:
“Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mahitaji ya Lawson yalikuwa Sh. 17,061,985,326, lakini Hazina ilipeleka Sh. 17,371,325,530, hivyo kuwa na ziada ya Sh. 309,340,200.”