BUNGENI: Polepole Aibuka na Tiba Asili Bungeni, Ataka Majaribio Dawa za Corona



SAKATA la tiba asili na tiba mbadala katika matibabu ya magonjwa ya upumuaji ikiwamo virusi vya Corona, limeibuka bungeni baada ya Mbunge mteule, Humphrey Polepole kuihoji Serikali kwamba ni lini majaribio ya dawa hizo yatafanyika. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)

Hatua hiyo imekuja huku kukiwa na minong’ono kwamba Serikali ya awamu ya sita imeweka kando tiba asili na mbadala katika kutibu ugonjwa huo baada ya ujio wa chanjo za Corona,

Hata hivyo, viongozi wa serikali walikana madai hayo na kusema tiba zote zitaendelea kutumika katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Akiuliza swali hilo leo tarehe 2 Februari, bungeni jijini Dodoma, Polepole amehoji, je, Serikali ina mpango gani na lini itaanza kuwezesha majaribio ya kitabibu kwa bidhaa za mimea dawa ambazo zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Mbadala?


Ameongeza tayari dawa hizo zinatumika kwa uhiyari wa wagonjwa na zimeonesha ufanisi mkubwa katika kutibu magonjwa mbalimbali yakiwemo ya mfumo wa upumuaji.

Akijibu swali hilo dogo la nyongeza, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel amesema tayari Serikali imekuwa ikifanya majaribio ya dawa hizo.

Amesema kupitia Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini – NIMR kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikifanya majaribio hayo.


“Katika fedha hizi za mkopo nafuu kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo jumla ya Sh trilioni 1.3 zilipokewa na Serikali, kati yake Sh bilioni 6.1 zilitengwa kwa ajili ya tafiti ikiwamo suala la tiba asili.

“Kama mnakumbuka hapa bungeni niliwahi kusema Rais alipeleka sh bilioni 1.2 pale NIMR kwa ajili ya kufanya mambo kama haya ambayo Mbunge ameulizia,” amesema.

Dk. Mollel amesema Rais Samia ameielekeza wizara kutoa kipaumbele kwenye eneo hilo la utafiti wa dawa za asili.

“Kwa sababu yametusaidia sana kipindi tunapitia wakati mgumu wa Corona… wakati hakuna anayejua suluhu ni nini kwenye tatizo hili,” amesema

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad