Dar es Salaam. Daraja la Tanzanite maarufu kama New Selander lililoanza kutumika jana limetajwa kuwa kivutio kingine cha utalii kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Daraja hilo lenye urefu wa kilomita 1.03, lina njia nne za magari na njia mbili za watembea kwa miguu, limejengwa pamoja na barabara unganishi zenye wa kilomita 5.2 na linaunganisha Hospitali ya Aga Khan na barabara za Obama, Kenyatta na Toures.
Wakizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya wananchi walisema ujenzi wa daraja hilo unaongeza vivutio vingine vya utalii baada ya lile la Kigamboni, kwani ujenzi wake ni wa kisasa na wa kuvutia.
“Mtindo wake wa ujenzi kuanzia kwenye nguzo, taa za pembeni na mahala pa kupumzikia ni mojawapo ya vionjo vinavyoongeza mwonekano mzuri wa daraja hilo,” alisema Mohamed Saleh, mkazi wa Dar es Salaam.
Katika daraja hilo kuna sehemu maalumu ambako mtembea kwa miguu anaweza kujikinga na mvua au jua.
“Sasa tuna daraja la pili katika Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam baada ya lile linalounganisha Kigamboni na Kurasini. Serikali inastahili pongezi kwa hili,” alisema Salehe.
Kupunguza foleni
Kwa upande mwingine, matumizi ya daraja hilo jipya yanatajwa kupunguza foleni ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Siku ya kwanza ya matumizi ya daraja hilo, ahueni imeonekana kwa wakazi hao kwa barabara hiyo kutokuwa na foleni kama ilivyozoeleka baada ya magari mengi binafsi kutumia daraja hilo.
Daraja hilo lililogharimu takribani Sh243 bilioni likifadhiliwa na Serikali ya Korea Kusini na kujengwa na kampuni ya ujenzi ya GS E&C, lilianza kujengwa mwaka 2018.
“Huwa tunashuhudia foleni kubwa asubuhi mpaka saa 5 hivi na jioni, lakini leo tangu kuanza kutumika daraja hakuna foleni, zimekuwa zikipita daladala na magari binafsi machache, wengi wamepitia Masaki daraja jipya ili wafike Posta kwa haraka,” alisema James Gunga, dereva bodaboda eneo la Palm Beach.
Mwananchi pia ilishuhudia waenda kwa miguu na wapanda baiskeli wengi wakitumia daraja hilo kutoka katikati ya jiji kuelekea hadi Oysterbay.
“Kabla ya daraja hili ilinibidi niwe napanda daladala kutoka mjini. Sasa hivi natembea kwa miguu hadi Coco Beach ninakofanyia biashara zangu. Ni kama dakika 25 hivi,” alisema Mfaume Juma.
Raisa Alex, mkazi wa Mbagala anayefanya kazi za ndani eneo la Masaki, alisema kabla daraja halijajengwa ilimlazimu kupanda magari mawili, lakini sasa akifika mjini hana haja ya kupanda gari lingine kwenda Masaki. “Kwa ukweli mimi daraja hili limenipunguzia nauli,” alisema Raisa.
Akizungumza wakati akikagua daraja hilo Januari 30, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema daraja hilo linalokatiza katika bahari ya Hindi litakuwa suluhisho la changamoto ya msongamano wa magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi. Aliwataka wananchi kulitunza daraja hilo na kwamba Serikali itasimamia jambo hilo, ili kama daraja limesanifiwa kuishi miaka 100, Watanzania walitunze liishi miaka 125.