DOUGLAS MUTUA: Putin ni hatari, sharti viongozi duniani washirikiane kumdhibiti



AMA kweli, kila soko lina mwendawazimu!

Wakati huu ambapo takribani dunia nzima inamuambaa Rais Vladimir Putin wa Urusi kama jini, Sudan inakimbia kushauriana naye.

Sudan imefanya hivyo wakati huu ambapo mataifa yanayoendelea, hasa Kenya, yametokea kuielimisha dunia kuhusu maovu ya mataifa makubwa kuyavamia madogo.

Putin anasutwa kwa kukiuka sheria za kimataifa na kulivamia taifa jirani la Ukraine huku akitoa visingizio vya kila aina, jambo ambalo limeyaudhi mataifa tajiri duniani.

Kenya na Ghana ni miongoni mwa mataifa yanayoendelea ambayo yameungana na yale ya magharibi pamoja na Amerika kulaani hatua ya Rais Putin.


 
Hilo lilithibitika mapema wiki jana Balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa, Bw Martin Kimani, alipotoa hotuba ya kupigiwa mfano akimkashifu Putin, ikasifiwa mbali na karibu.

Lakini hata kabla ya kelele za ushangilizi huo kufifia, serikali ya kijeshi ya Sudan iliwatuma wajumbe wa ngazi ya juu, miongoni mwao naibu kiongozi wa nchi, kushauriana na Putin kuhusu ushirikiano wa mataifa yao.

Hiyo ni hatua hatari mno wakati ambapo watu wanahofia huenda vita vikuu vya dunia vikazuka kwa mara ya tatu.


Kisa na maana? Hatua yenyewe inaweza kuzishawishi serikali nyingine za kijeshi duniani kuanzisha ushirikiano na Urusi ili Putin azidumishe mamlakani.

Kwa muda mrefu, Putin ametamani sana kuigawa dunia kati ya mataifa yanayoiunga mkono Urusi na yale yanayofungamana na Marekani pamoja na mataifa ya magharibi.

Hakufurahishwa na kuvunjika kwa Muungano wa Kisoshiolisti wa Usovieti (USSR) kulikoiacha Marekani pekee ikinguruma kama simba duniani kwa mafedha, nguvu za kijeshi na ushawishi.

Ni kwa kusudi la kuupinga ushawishi huo ambapo Putin ametishia tangu mwaka 2021 kuivamia Ukraine, anayosisitiza isijiunge na shirika la kijeshi la NATO.

Pia, amejaribu kuishinikiza Amerika iondoe majeshi yake eneo la mashariki mwa Uropa akidai yanatishia usalama wa taifa lake.

Masharti hayo yamekataliwa kabisa, sikwambii amewekewa na vikwazo, lakini mja huyo jeuri na kaidi amevamia Ukraine liwe liwalo! Na si kuvamia tu! Ametishia iwapo taifa lolote litaingilia kati, atalishambulia pia na kulisababishia uharibifu mkubwa. Na vyake si vitisho tu, anaweza kutenda hayo.

Dunia ingali na fursa ya kutumia diplomasia kutatua mzozo huo, hasa kumshawishi Putin aondoe majeshi yake Ukraine.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad