DPP: Ushahidi ulikuwa dhaifu mauaji ya askari



Dar/Moshi. Sakata la mauaji ya askari polisi Linus Nzema limechukua sura mpya baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kueleza kuwa alipelekwa ushahidi unaojikanganya.

Akizungumza juzi jioni na Mwananchi, DPP Sylvester Mwakitalu alisema alifikia uamuzi wa kutomshtaki askari aliyehusishwa na mauaji hayo kutokana na udhaifu huo wa ushahidi kwenye jalada la uchunguzi.

Alisema alichokikuta kwenye jalada hilo ni mkanganyiko mtupu wa maelezo ya mashahidi.

Mzema aliuawa kwa risasi na askari mwenzake Mei 31, mwaka jana nje ya baa ya Ndafu, iliyopo Kijiji cha Kituri wilayani Mwanga, wakati yeye na askari wenzake wakijiandaa kurejea kituoni baada ya kumaliza operesheni ya kusaka mirungi.


 
Kauli ya DPP inajibu maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Simon Maigwa kuwa jalada la shauri hilo lilikwenda kwa DPP na ikaonekana hakuna jinai, kauli iliyopingwa na wanasheria na watetezi wa haki za binadamu kuwa si jambo la kawaida kwenye kesi za mauaji.

Kwanini hakufungua kesi

Akizungumza na Mwananchi juzi jioni, DPP Mwakitalu alisema aliamua kutofungua kesi kwa sababu kwenye jalada la uchunguzi kulikuwa na mkanganyiko wa maelezo ya mashahidi.

Alisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani mtuhumiwa na hivyo asingeweza kumpeleka mtu mahakamani bila ushahidi wa kutosha.


“Jalada lililetwa kwangu kweli na tukalipitia, tuliona hatuna ushahidi wa kuthibitisha makosa ya mauaji. Unajua makosa ya mauaji ni makubwa. Ukimshtaki mtu akitiwa hatiani maana yake anahukumiwa kunyongwa,” alisema.

DPP alisema kosa la mauaji bila kukusudia na kosa la mauaji ya kukusudia, ushahidi wake hautofautiani kwa sababu yote ni makosa makubwa ambayo lazima uwe na ushahidi wa kosa kutendeka.

“Jalada tuliloletewa halikuwa na huo ushahidi wa kutosha. Hatuwezi kwenda mahakamani kwa kesi ambayo tunajua tunakwenda kushindwa. Ni embarrassment (fedheha) kwetu, lakini pia kwa huyo mnayem-suspect (mnayemtuhumu),” alisema DPP.

“Makosa kama ya mauaji unajua hayana dhamana. Ukishamtuhumu mtu na ukampeleka mahakamani, akakaa miaka mitano na kesi ikaja kuamuliwa kuwa hakuna ushahidi, utakuwa umemtendea kitu ambacho si sawa,” alieleza.


 
Akizungumzia yaliyomo kwenye jalada hilo, Mwakitalu alisema tukio hilo lilitokea mahali ambako kwanza ilikuwa ni usiku na kuna habari za mashuhuda, wakiwamo askari wenyewe, ambazo zinaacha mkanganyiko.

“Kuna mtu mmoja anaandikwa kwenye maelezo pale lakini anatoa statement (maelezo) ambazo mimi nikizisoma na ushahidi mwingine zinaji-contradict (zinajichanganya).

“Kuna version kama tatu, nne kwenye lile jalada. Ya kwanza huyo mtu alipigwa risasi akiwa nje ya gari. Ya pili, alipigwa risasi akiwa ndani ya gari, kwamba askari walikuwa wanagombania kukaa seat (kiti) ya mbele,” alisema.

Vilevile, DPP aliongeza kuwa kuna shuhuda mwingine anasema aliona askari wanajibizana kisha mmoja akakoki risasi akampiga mwenzake.


“Stori ya tatu ni kwamba alijigonga kwenye gari na stori ya nne ni kwamba alianguka kwenye bodaboda. Sasa unaona, hayo yote yako kwenye jalada moja, sasa hapo mimi naendaje mahakamani?” alihoji Mwakitalu.

Mkurugenzi huyo, alisema “tukipata nafasi mimi naweza kuwapa access (kuwaonyesha) ya kilichomo katika jalada, bahati mbaya nimeshalirudisha Moshi, lakini nalifahamu hilo kwa sababu lilifika kwangu kabisa wala si kwamba watu wangu ndio walilifanyia kazi, hayo maamuzi ni ya kwangu mwenyewe.”

DPP alisisitiza kuwa kwa sasa ameamua kuwa atakwenda mahakamani pale ambapo ana ushahidi kwa kesi zote zinazopelekwa kwake.

“Kwanza kuna vitu vingi ambavyo tutaviokoa hapo.Ile unampeleka mtu mahakamani halafu anakuja kushinda kesi, ile dhana ya kwamba alibambikiwa huwezi kuikwepa.

“Lakini unawapeleka watu mahakamani kwa makosa ambayo hayana dhamana, wanakaa mahabusu wanarundikana kule, msongamano unakuwa mkubwa na mwisho wa siku hamuwezi kushinda kesi.


 
Katika kusisitiza msimamo huo, Mwakitalu alisema wameamua kurekebisha sheria, ili iwe bayana kwamba watapeleka kesi mahakamani pale ambapo wataakuwa na ushahidi wa kutosha.

Alisema mapendekezo ya marekebisho hayo yalishasomwa mara ya kwanza katika Bunge la Novemba na anadhani kwenye Bunge hili (linaloendelea) yatapitishwa kuwa sheria.

“Kwa hiyo pale ambapo mimi sioni nina ushahidi wa kutosha sitakwenda mahakamani kwa kesi zote, si kesi hiyo moja tu,” alisema DPP.

Alichoeleza RPC Moshi

RPC Maigwa alisema askari wakiwa kweye operesheni mpakani walikuwa wameweka risasi chemba na zile silaha zilikuwa kwenye kiti.

Alisema wakati dereva amepanda anataka akae vizuri kwenye kiti, kumbe akavuta trigger (usalama) risasi ikaenda ikam shoot (kumpiga) yule bwana (Mzema).”

“Kwa hiyo ilipochunguzwa, tukapeleka (jalada) kwa mwanasheria (DPP) ikaonekana criminalities (ujinai) haupo, ikaonekana ni uzembe. Kwa mazingira haya hakuna nia ovu. Ni sawa na ajali,” alilieleza Maigwa.

Wakati RPC akieleza hayo, mama wa marehemu, Lucia Mkepule na mjomba wa marehemu, Atilio Kalinga, walimuomba Rais Samia Suluhu Hassan aingilie kati suala hilo ili kamati aliyoagiza iundwe na Waziri mkuu kuchunguza mauaji ya Mtwara na Kilindi iende pia Mwanga kuchunguza mauaji ya mwanaye kwa kuwa pia tukio zima linahusisha polisi kujichunguza.

Maelezo ya mashuhuda

Mashuhuda wa tukio hilo ambao walizungumza na Mwananchi kijijini Kituri mara baada ya mauaji hayo, walidai kushuhudia polisi mmoja wanayemjua kwa sura na jina kuwa ndiye aliyemfyatulia mwenzake risasi ya shingo.

Mmoja wa mashuhuda hao kati ya wanne, alidai walikwenda katika baa ya Ndafu baada ya polisi kuwataka wafike hapo ‘wamalizane’ ili rafiki yao aliyekuwa amekamatwa na viroba sita vya mkaa aachiwe.

“Mwanzoni tuliambiwa tulipe 500,000 ili aachiliwe tukawaambia hatuna hiyo hela, yule mwenzake (na marehemu) akasema tumpe 200,000. Marehemu akasema tutoe Sh100, 000. Walikuwa askari wengi wakatufukuza tutoke nje kwanza. Tulikaa nje ya geti tukawa tunawasikilizia na tulishuhudia askari alikwenda nyuma ya dereva akachukua bunduki akampiga nayo Linus shingoni. Huyo polisi akaanza kusema “nimeua, nimeua” huku akiwa ameweka mikono kichwani.

“Tulimsikia na kumuona dereva wa lile gari la polisi akawapigia simu wenzake, ambao walikuwa tayari wameshaondoka pale kwenye ile baa, akawaambia mlipokuwa huko porini mliacha risasi chemba? Amemuua Linusa.

“Wakati huyo polisi mwenzake ‘akisema nimeua, nimeua’ sisi tuko nje ya geti walikuwa, hawajui kama tunawaona. Wahudumu baa waliambiwa wasimwambie mtu yeyote kilichotokea wakati huo sisi tunasikia kila kitu na tunawaona kwa nje.”

Shuhuda mwingine alidai muda mfupi polisi wengine walikuja na kuubeba ule mwili wakauweka kwenye gari lile ambalo marehemu na polisi mwenzake walikuwa wanazozana na kuondoka nao.

“Nimeshuhudia tukio hilo na mwenzangu niliyekuwa naye na pale baa walikuwepo wahudumu wawili,” alidai shuhuda huyo ambaye kama wenzake waliomba jina lisitajwe gazetini.

Taarifa ya awali polisi ilisema pikipiki ya wauza mirungi ilimgonga Nzema na kumsababishia majeraha maeneo ya shavu la kulia, puani na miguuni na alipelekwa Kituo cha Afya cha Kileo kwa matibabu lakini akafariki dunia wakati akipatiwa matibabu, suala ambalo baada ya uchunguzi ilibainika haikuwa kweli.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad