Dodoma. Mbunge wa Nzega Vijijini, Dk Hamisi Kigwangalla, juzi aligonga mwaka bungeni baada ya kutaka kujitetea kuhusu madai ya kutumia vibaya madaraka alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.
Dk Kigwangala (pichani) aliacha kuchangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Mashirika ya Umma (LAAC), badala yake alianza kueleza namna alivyotajwa kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Dk Kigwangala alisema kuanzia sasa hatonyamaza milele, kwani ameonewa na kuchafuliwa sana wakati yeye ni mzalendo hivyo inabidi kueleza ukweli popote.
Hata hivyo, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson alimtaka mbunge huyo kuacha kuzungumza jambo ambalo halikuwasilishwa kwenye taarifa za kamati hizo badala yake ajikite kwenye taarifa.
Spika alisema ikiwa mbunge huyo atakuwa na jambo la kuzungumza katika kile anachodhani ameonewa, basi anayo nafasi ya kupeleka taarifa zake sahihi na Bunge kuzifanyia kazi.
“Hiki unachokisema hakimo humu, sijui unakitoa ukurasa wa ngapi, Sasa unatumia dakika hizi kukanusha jambo ambalo halipo humu, kama unadhani CAG alikuonea niletee malalamiko nitafanyia kazi,” alisema Dk Tulia.
Hata hivyo, alipotakiwa kuendelea na mchango wake, Dk Kigwangala alinyoosha mikono juu ishara ya kuwa hana cha kuchangia tena na kuruhusu mbunge mwingine aendelee.
Sakata lenyewe
Katika ripoti iliyowasilishwa bungeni na CAG April 6, 2022 ukurasa wa 256 kifungu cha 13 kifungu kidogo 212, CAG alimtaja Dk Kigwangala kwa jina kuwa alikuwa ametumia vibaya madaraka yake na kusababisha upotevu wa fedha bila maelezo.
CAG alisema Dk Kigwangala alisababisha hasara ya Sh2.08 bilioni katika tamasha la Urithi Festival kwa kuwalipa wasanii lakini hakukuwa na maelezo sahihi.
Mbali na hilo taarifa hiyo ilimtaja Dk Kigwangala kwamba alitumia vibaya Sh171 milioni kwa ajili ya safari binafsi ya kupanda Mlima Kilimanjaro na kwamba alilazimisha fedha hizo zitolewe kwenye mashirika yaliyo chini ya wizara.
Akitoa ufafanuzi nje ya ukumbi wa Bunge, waziri huyo wa zamani wa Maliasili na Utalii alisema kuwa taarifa zote zilikuwa ni uongo, ambao ulilenga kumchafua kisiasa na kumgombanisha na mamlaka za uteuzi.
Alisema wakati hayo yanatokea yeye alikuwa amelazwa hospitalini kutokana na ajali aliyoipata Agosti 4,2018 hivyo kuna wizarani walioanza kutumia nafasi hiyo kummaliza kisiasa.