Shirikisho la kandanda duniani, Fifa, Alhamisi hii limeipiga marufuku Kenya na Zimbabwe kushiriki katika shughuli zote za kandanda kutokana na hatua ya serikali kuingilia masuala yake.
Rais wa Fifa Gianni Infantino amethibitisha kusimamishwa kwa muda kwa shughuli zote za soka wakati wa mkutano na wanahabari wa baraza la Fifa.
“Bila ya kuathiri uchunguzi wowote wa mamlaka ya kitaifa au vyombo vingine vya mahakama, baraza la Fifa pia liliamua kusimamisha Shirikisho la Soka la Kenya na Chama cha Soka cha Zimbabwe mara moja kutokana na kuingiliwa isivyofaa na serikali ,” Infantino alisema.
Waziri wa michezo nchini Kenya Amina Mohammed , tarehe 11 Novemba mwaka uliopita alilifutilia mbali shirikisho la soka nchini Kenya FKF lililokuwa likiongozwa na Nick Mwendwa na badala yake kuunda kamati simamizi, miongoni mwa masuala mingine , ili kuendesha soka kulingana na katiba ya shirikisho hilo.