Ndege ya kivita ya Ukraine, MiG-29 Fulcrum inayoongozwa na rubani aliyebatizwa jina la The Ghost of Kyiv (Mzimu wa Kyiv), imepata umaarufu mkubwa kutokana na oparesheni za kijeshi inazozifanya katika Jiji la Kyiv ambapo mpaka sasa inadaiwa kuziangusha ndege sita za kivita za Urusi.
Inaelezwa kwamba ndege sita za Urusi zilitunguliwa Februari 24, 2022 muda mfupi baada ya Urusi kuanza mashambulizi ya anga dhidi ya serikali ya Ukraine na kuanzia hapo, The Ghost of Kyiv amepata umaarufu mkubwa na kuungwa mkono na wananchi wengi wa Ukraine.
Ndege za Urusi zilizotunguliwa na kuthibitishwa na Mkuu wa Majeshi wa Ukraine, Valerii Zaluzhnyi ni pamoja na ndege mbili za kijeshi za Su- 35, ndege mbili za kijeshi za Su-25, ndege moja ya Su-27, ndege nyingine ya МіG-29 ambazo zote zilitunguliwa katika saa 30 za kwanza tangu mashambulizi yaanze jijini Kyiv mhusika mkuu akiwa ni The Ghost of Kyiv.
Ili kuthibitisha kwamba ni kweli rubani huyo yupo na si uzushi wa mitandaoni, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine amekaririwa akieleza kwamba rubani wa ndege hiyo ambaye jina lake halisi halijawekwa hadharani, ni miongoni mwa marubani kadhaa wa ndege za kivita wa Ukraine, ambao waliamua kurudi nyumbani kuisaidia nchi hiyo dhidi ya uvamizi wa Ukraine.
Rais wa zamani wa Ukraine, Petro Poroshenko kupitia akaunti yake ya Twitter, ameposti picha ya rubani wa ndege moja ya kivita ya Ukraine, na kueleza kwamba huyo ndiyo Ghost of Kyiv anayewatoa kimasomaso wananchi wa Ukraine katika kuikabili Urusi.
Inazidi kuelezwa kwamba tangu kuanza kwa vita hiyo, Ghost of Kyiv ameendelea kufanya doria za anga usiku na mchana, akiziwinda ndege za Urusi katika anga la Ukraine.