Inasemekana...Rayvanny Amekwama Kuondoka Wasafi



KUMEKUWA na tetesi nyingi kuwa msanii Raymond Mwakyusa au Rayvanny yupo mbioni kuondoka kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na Diamond Platnumz.


Tetesi hizo zilipaswa moto na mmoja wa mameneja wa WCB, Mkubwa Fella alipoeleza kuwa kuna msanii anapanga kuondoka kwenye lebo hiyo, jambo lililosababisha wengi kuamini ni Rayvanny kutokana na kuanzisha lebo yake ya Next Level Music (NLM).


Hata hivyo, meneja mwingine wa WCB, Sallam SK alikanusha kuwa siyo Rayvanny bali ni Hanstone. Hadi sasa WCB yenye wasanii sita, tayari wasanii wawili wamejitoa ambao ni Rich Mavoko na Harmonize.


Hanstone ambaye alipata umaarufu na Wimbo wa Iokote alioshirikiana na Maua Sama, inadaiwa alikuwa amesainiwa na lebo hiyo, lakini akaamua kuachana nayo kwa madai ya ucheleweshwaji wa kutoka.



Hata hivyo, habari za ndani zinadai kwamba, tetesi za Rayvanny kuondoka WCB ni za kweli, lakini amekwama kwa madai kwamba kuna kiwango cha pesa ambacho anapaswa kulipa WCB ili akubaliwe kuondoka kisheria.


Madai mengine ni kwamba, kama Rayvanny analazimisha kuondoa WCB, basi ingemlazimu kuacha kazi alizozifanya kwa maana ya nyimbo zote.


Vilevile inasemekana ingemlazimu kuacha akaunti za mitandao ya kijamii anazomiliki ikiwemo chaneli yake ya Mtandao wa YouTube ambayo ina wafuasi milioni 3.5.



Safari ya Rayvanny si nyepesi kama wengi wanavyoamini.

Data zilizo kwenye makabrasha ya Gazeti la IJUMAA zinaonesha Rayvanny alikuwa akifanya muziki wa rap kabla ya kuanza kuimba mwaka 2011 akiibuka mshindi katika mashindano ya free style pale Coco Beach jijini Dar.


Wakati huo alijulikana kama Raymond, akatafuta nafasi ya kutoka kimuziki chini ya Tip Top Connection chini ya Babu Tale. Aprili, 2016 alisainiwa kwenye Lebo ya WCB na kutoa wimbo wake wa kwanza wa Kwetu uliofanya vizuri.


Usiku wa Juni 25, 2017 katika ukumbi wa Microsoft Theater Centre, Los Angeles nchini Marekani, Rayvanny alipokabidhiwa Tuzo ya BET kupitia Kipengele cha Viewer’s Choice Best New International Act na kuwa msanii wa kwanza na pekee kutoka Tanzania kushinda tuzo hiyo hadi sasa.



Diamond amewania Tuzo za BET zilizoanza kutolewa Juni 19, 2001 mara tatu bila ushindi wowote, alifanya hivyo mwaka 2014, 2016 na 2021. Hivyo Rayvanny ni msanii wa pili Afrika Mashariki kushinda tuzo hiyo baada ya Eddy Kenzo wa Uganda.


Ferbruari, 2020, Rayvanny aliachia Extended Playlist (EP) yake ya kwanza ya Flowers iliyofanya vizuri hadi kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya kujadiliwa (consideration) kwa ajili ya kuwania Tuzo za Grammy.


Mwaka mmoja baadaye, Februari 1, 2021, Rayvanny aliachia albam yake ya kwanza ya Sound From Africa ikiwa na nyimbo 23 alizowashirikisha wasanii 20 kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika.


Sound From Africa iliweka rekodi Afrika Mashariki kwa kufikisha wasikilizaji (streams) zaidi ya milioni 100 ndani ya wiki moja.



Rayvanny akiwa chini ya WCB, Machi, 2021 alizindua lebo yake ya Next Level Music (NLM) akiwa ni msanii kwanza kufanya hivyo kwani Rich Mavoko na Harmonize waliondoka WCB ndipo wakaanzisha lebo zao.


Septemba 24, 2021 alimtoa msanii wake wa kwanza, Mac Voice ambaye ameachia EP ya My Voice yenye nyimbo tano ambapo amemshirikisha Rayvanny katika nyimbo mbili, nayo ilifanya vizuri hadi kufikisha wasikilizaji zaidi ya milioni 10 kwenye mitandao ya iTunes, Spotify, Audiomack na Boomplay na Play Music kwa kipindi cha mwezi mmoja tu.


Wakati Mac Voice akiendelea kufanya vizuri, Oktoba 29, 2021 Rayvanny aliachia EP yake ya pili ya New Chui yenye nyimbo sita huku akimshirikisha msanii mmoja ambaye ni Abby Chams.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad