Inonga arudisha mkwanja Yanga, amkimbia Mayele Airport



MSIMU huu mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba walimsajili kibabe beki wa kati, Henock Inonga Baka ‘Varane’ kutoka DC Motema Pembe ya Ligi Kuu DR Congo kwa mkataba wa miaka miwili.

Usajili wa Inonga ulikuwa wa kibabe kutokana na wapinzani wao, Yanga, awali kumalizana kwa kiasi kikubwa na mchezaji huyo, lakini mwisho wa Simba wakapindua meza na kumnyakua beki huyo.

Inonga amefanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti akizungumzia picha hilo jinsi lilivyokuwa mpaka kuachana na Yanga kwenda kukipiga katika kikosi cha Simba alichonacho hadi sasa.

KUTUA YANGA

Kabla ya kutua katika kikosi cha Simba mwanzoni mwa msimu huu, Yanga ndio waliokuwa wa kwanza kuhusishwa na kumtaka Inonga ambaye alikuwa anakuja kuongeza nguvu katika eneo la ulinzi.


 
Inonga anasema kabla ya kuhitajika na Simba, Yanga walikuwa wa kwanza kumtafuta na kuna mmoja wa viongozi aliongea naye tena na mazungumzo yalifika mbali kwa kukubaliana kila kitu.

Anasema akiwa katika hatua za mwisho kufanya uamuzi Yanga alipokea simu kutoka kwa kiongozi mwingine wa juu wa Simba ambaye naye alimueleza kuhitajika katika timu hiyo huku wakimuwekea maslahi makubwa mezani kuliko yale ya Yanga.

“Nikiwa katika tafakari ya kufanya uamuzi tena muda huo nikiwa nimepima mpaka Uviko 19 na pesa iliyotumwa na Yanga, nilifanya mawasiliano na wachezaji wa DR Congo waliokuwa hapa nchini,” anasema Inonga na kukiri kwamba baada ya kufika nchini alilazimika kurejesha fedha za Yanga walizomtumia kulipia gharama za kupima Uviko. Kuhusu tiketi ambayo Yanga walikuwa wamemtumia anasema kwamba hakulazimika kuilipa kwavile hakuitumia, alisafiria tiketi ya Simba kuja Dar es Salaam. “Katika kufanya mawasiliano wenzangu waliokuwapo hapo na hata waliowahi kucheza waliniambia Simba ni bora kuliko Yanga kwa wakati ule, kwa hiyo nilibadili uamuzi na kuamua kutua Msimbazi.”


Inonga anasema Yanga walifanya kila kitu kwa ajili yake na walikuwa wanamsubiri nchini ili kuja kumalizana nao kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili.

“Dah! Nadhani ilikuwa imepangwa tu nije kucheza Simba kwani nilifika mpaka uwanja wa ndege wa Kinshasa ili nije Tanzania, lakini hilo lilishindikana na nilibadili uamuzi na kuja siku nyingine kwa ajili ya Simba,” anasema.

“Sikuweza kupokea wala kuwasiliana tena na Yanga baada ya siku niliyotakiwa kuja nchini kwa ajili yao kushindwa kufanya hivyo na nadhani wao walikuja kuona tu natambulishwa Simba.

“Haukuwa uamuzi rahisi kwani nilifika mpaka uwanja wa ndege, ila kutokana na sababu za msingi niliamua tu kubadili ule wa awali na kufanya uamuzi ya pili kuja katika kikosi cha Simba.”


 
AMKIMBIA MAYELE

Inonga anasema wakati anatakiwa kuja Tanzania kujiunga na Yanga walikuwa na tiketi sawa za ndege na Fiston Mayele na wote walikutana uwanja wa ndege kabla ya kuingia ndani.

Anasema wakati mwenzake akimtangulia ndani kukaguliwa ndipo alipobadili uamuzi baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa msimamizi wake pamoja na Simba kwani walijua angetua na Mayele biashara ingemalizikia Jangwani.

“Kama unakumbuka ile mechi ya Yanga nilicheza kwa ushindani mkubwa dhidi yake na kuhakikisha hawezi kuleta hatari yoyote langoni kwani ni straika mzuri mwenye uwezo wa kufunga,” anasema Inonga.

“Mbali ya hivyo tumejuana tangu Congo kwa maana hiyo lazima kulikuwa na ushindani kati yetu kila mmoja akitaka kuisadia timu yake kushinda, lakini mbali ya masihara yetu pale uwanjani pamoja na ushindani mwisho wa mechi tuliongea na maisha mengine kuendelea.”


MWANASPOTI LAMUIBUA

Inonga anasema alifika nchini kwa usiri mkubwa siku mbili mbele baada ya ile ambayo alikubaliana na Yanga, ambapo alikwenda kuwekwa katika jengo moja katikati ya jiji na hakuna aliyekuwa anafahamu juu ya uwepo wake nchini.

“Tena umenikumbusha yaani ninyi Mwanaspoti mliniandika kwenye gazeti lenu sijui taarifa mlipata wapi kama nimekuja nchini kwa ajili ya Simba na kuachana na Yanga,” anasema beki huyo.

“Unajua kwa nini nimekumbuka hilo. Wakati nasaini Simba niliambiwa kuna mwandishi huku (Tanzania) nimeongea naye huku naonyeshwa gazeti lenu mbele kukiwa na picha yangu. Mkaona haitoshi siku nyingine mkanifuata na hospitali kunipiga picha kabisa.

“Hongereni mlifanya kazi nzuri kwani jambo langu lilikuwa na usiri mkubwa ndani yake.”

Anasema baada ya kutua Simba kuna malengo alijiwekea na kati ya hayo kuna yaliyotimia kama kutamani kuwepo katika kikosi cha kwanza na kucheza mara kwa mara ili kutoa mchango katika timu.


 
“Baada ya kutua Simba nimejifunza vitu vingi kama mazingira mapya na vitu mbalimbali ambavyo katika maisha yangu ya soka kule Congo sikuwa nakutana navyo kama ilivyo, hapa nchini kumekuwa na mzuka mkubwa wa mashabiki wa soka katika kila uwanja ambao Simba tunakwenda kucheza. Ligi ina ushindani wa kutosha hakuna timu ndogo inayokubali kufungwa kwa urahisi.

“Baada ya kutua Simba kuna vitu kama faida katika maisha yangu nimefanikiwa hata yale ya nje ya uwanja pengine kama nisingekuwa katika klabu hii kubwa labda nisingeyafikia mafanikio hayo.”

WAKONGO YANGA

“Nimeishi na wachezaji wa DR Congo katika timu nyingine ni nadra kuona wachache wanaishi vizuri, ila uwepo wa wengi katika timu moja kwa kiasi kikubwa kuna changamoto inaweza kutokea katikati yenu,” anasema.

“Ukitaka kuamini hili ambalo nalieleza kaa chini na Mukoko Tonombe muulize hili ambalo nasema anaweza kukueleza vizuri ndio maana nami nilifanya uamuzi baadaye ingawa Yanga ni timu kubwa Afrika.”

BEKI BORA DR CONGO

Kwenye tuzo za Ligi Kuu ya DR Congo msimu uliopita Inonga alichaguliwa beki bora wa msimu kutokana na kiwango bora alichoonyesha katika kikosi cha DC Motema Pembe na mpaka kuitwa timu ya taifa kwa wachezaji wa ligi ya ndani.

Inonga anasema miongoni mwa deni alilokuwa nalo ni hilo Simba wamevutiwa na kiwango chake bora mpaka kutumia nguvu ya kutosha ili kumsainisha mkataba kukipigania kikosi hicho kwenye mashindano yote.

“Kama nilifanikiwa kucheza Congo na kuwa mchezaji bora natakiwa kulifanya hilo hapa kwani nikiweza kucheza katika kiwango cha juu sio mafanikio yangu binafsi, bali nitaisaidia timu kufikia malengo,” anasema.

“Nataka kucheza katika kiwango cha juu katika kila mechi kwani hiyo ndio silaha ya timu yangu kufanya vizuri na ndipo nitaendelea kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza mara kwa mara hayo mengine yatakuja tu.”

HADI KIPA FRESHI

Inonga anasema katika uwanja anaweza kucheza nafasi zote hadi kipa na hicho ni kipaji alichonacho tangu utotoni akicheza soka ambalo halikuwa la ushindani. “Katika makuzi yangu na maisha ya soka nimecheza kwenye nafasi zote uwanjani na ikitokea siku tumepata shida inayolazimisha mchezaji akae kipa nafasi ya Aishi Manula kama nipo uwanjani naenda kucheza tena vizuri bila shida,” anasema.

“Watu wengi hawafahamu kama naweza kucheza kwenye nafasi nyingi uwanjani kwani ukiangalia katika timu ya DC Motema Pemba na FC Renaissance nimecheza katika nafasi nyingi tofauti mbali ya beki wa kati tu.”

MATAJI MENGI

Inonga anasema kutokana na ukubwa Simba ulivyo alivyoambiwa kabla ya kusajiliwa pamoja na malengo ya timu hiyo, wanastahili kupata mataji mengi kwenye mashindano tofauti.

Anasema Simba ni aina ya timu yenye malengo makubwa na inataka mataji mengi katika kila kombe walilopo wakitamani kulichukua ili kuonyesha ukubwa wao.

“Hatukuanza msimu vizuri kwa kukosa Ngao ya Jamii, lakini tumechukua Mapinduzi na tumepanga kufanya hivyo kubebea Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (ASFC) na kufanya vizuri zaidi katika Kombe la Shirikisho Afrika,” anasema.

“Hakuna siri kubwa zaidi ya kwetu wachezaji kujituma kama nilivyosema hapo awali ili tuweze kuchukua mataji hayo kwani sio kazi rahisi, tunatakiwa kupambana na kujituma zaidi ya wakati huu.

“Tunaomba mashabiki wetu waendelee kuwa nasi katika kila mashindano ambayo tutakuwepo ili kufanikisha jambo hilo la kuchukua mataji kwani ni ya wachezaji wenzangu ni hiyo.”

KWA NINI VARANE?

Inonga anazungumzia kwa nini amepachikwa jina la utani la beki wa kati wa Manchester United, Raphael Varane na mashabiki wa soka nchini DR Congo. “Hata nashindwa kuelewa unajua ilikuwaje? Msimu uliopita ndio nililipata hilo jina kutokana na kazi ambayo nilifanya uwanjani katika kila mechi mashabiki wakaanza kuniambia nacheza kama Varane,” anasema Inonga.

“Jina likaanza kukua kama utani vile wachezaji wenzangu ndani ya timu katika mazoezi wakaacha kuniita jina langu na kuniita Varane, mara likaanza kuwa kubwa kwa mashabiki nao wakawa wananiita hivyo.

“Nilishangaa kuna baadhi ya mechi mwanzoni kabla ya jina hili la Varane kuchanganya nikiokoa shambulizi, basi mashabiki kule jukwaani hunishangilia kwa kuniita jina hilo jipya.

“Mwisho wa siku hata katika mahojiano mbalimbali ya mashabiki wakaacha kuniita jina langu na kutumia hilo la Varane kutokana na ambavyo nacheza kufananishwa na beki huyo na jina hili lipo mpaka sasa Congo na ni maarufu.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad