WAMECHUKUA. Sadio Mane ameibeba Senegal baada ya kufunga penalti ya mwisho iliyowapa Senegal ubingwa wao wa kwanza wa fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 wakiilaza Misri kwa penalti 4-2 baada ya dakika 120 kuisha bila ya bao.
senegal pic 2
Kipa wa Senegal na klabu ya Chelsea, Edouard Mendy aliokoa penalti moja na nyingine ya Misri ikigonga nguzo, lakini kipa wa Misri, Mohamed Abou Gabal aliyeshinda tuzo ya nyota wa mchezo akiokoa moja.
senegal pic 3
Mbali na kuokoa hatari nyingi zilizoibakisha Misri mchezoni, kipa Abou Gabal anayekipiga katika klabu ya Zamalek ya nchini Misri, ndani ya dakika 10 za kwanza za mechi hiyo ya fainali aliokoa penalti ya Mane, iliyotokana na beki Saliou Ciss kuangushwa ndani ya boksi la Misri.
Shuti la Mane alilopiga upande wa kushoto lilipanguliwa kiufundi na kipa huyo, ambaye kabla ya kuokoa alionekana kupokea ushauri kutoka kwa mchezaji anayecheza na Mane kwenye klabu ya Liverpool, Mohamed Salah na akaruka upande sahihi.
Senegal, waliingia katika michuano hiyo wakipewa nafasi zaidi ya kutwaa ubingwa kutokana na kikosi chao kuundwa na wakali wengi wanaotamba Ulaya, akiwamo Mane, kipa Edouard Mendy, Kalidou Koulibaly, Cheikhou Kouyate, Idrissa Gana Gueye, Ismaila Sarr wakiwa chini kocha wao Aliou Cisse, ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo ya taifa.