WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema Dk. Mwele Malecela kabla ya kuchukua fomu kuwania kupitishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kinyang’anyiro cha urais 2015, alimfuata nyumbani kwake kumuomba ushauri. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Jaji Warioba ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika ibada ya kuaga mwili wa Dk. Mwele iliyofanyika leo tarehe 19 Februari, 2022 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Dk. Mwele (58) ambaye hadi umauti unamfika Tarehe 10 Februari, 2022, alikuwa Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyopewa Kipaumbele katika Shirika la Afya Duniani (WHO).
Akimueleza Dk. Mwele, Jaji Warioba amesema alikuwa akipata taarifa za Dk. Mwele kutoka kwa mwanaye anayefahamika kwa jina la Jane ambaye walisoma wote shule ya Skondari Weruweru mkoani Kilimanjaro.
Dk. Mwele Malecela, Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika vya Shirika la Afya Duniani (WHO)
“Mtu aliyekuwa akituambia hali yake ni Jane, alikuwa akiwasiliana naye na mara ya mwisho siku chache kabla ya kifo chake, alikuja kunieleza kuwa aliwasiliana na Dk. Mwele akawa na wasiwasi, ndipo akapata taarifa kuwa ametutuoka..
“Dk. Mwele alikuwa ni mtu anayejiamini, alijiamini sana, mwaka 2015 alikuja kwangu kutaka ushauri kama achukue fomu kugombea urais.
“Nikamwambia Mwele unaona una uzito wa kutosha kuingia katika kundi hili? akaniambia baba ( Mzee Samuel Malecela) naye amesema hivyohivyo, lakini mimi naamini naweza… kweli aliingia alikuwa ni mtu anajiamini hakuogopa kitu chochote.
Jaji,Joseph Warioba Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
“Mwele ametuachia legacy lakini tumemuona kwa utumishi wake, lakini legacy kubwa tumemuona kama binadamu alivyokuwa akiwalea wengine.
“Mwenyezi Mungu ameona ni wakati wake amchukue Dk. Mwele na tushukuru kwa maisha aliyompa hadi kufikia sasa,” amesema Jaji Warioba.