Jakaya Kikwete afichua sababu kumteua Dk. Mwele



RAIS mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete, amefichua siri ya kumteua Dk. Mwele Malecela mwaka 2010, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Rais mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete na mkewe, Mama Salma Kikwete, wakiweka shada la maua kwenye kaburi la aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Udhibiti wa Magonjwa ya Kitropiki Yasiyopewa Kipaumbele wa Shirika la Afya Dunia (WHO), Dk. Mwele Ntuli Malecela, baada ya mazishi yake, kijijini kwao, Mvumi, Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma, jana. PICHA: IBRAHIM JOSEPH
Dk. Mwele alifariki dunia Februari 10, mwaka huu, kwa saratani ya kichwa nchini Uswisi akiwa anafanya kazi Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele, Geneva Uswisi.

Akitoa salamu za pole kwa wanafamilia na mamia ya waombolezaji, alisema kilichomvutia ni ujasiri wake wa kuyasema magonjwa mbalimbali hususan matende na hakuwa na kigugumizi.

Alisema kuna wakati alimwambia huogopi kuyasemea na alimjibu ndiyo kazi yetu kusema na kwamba lazima kuyataja yalivyo.

“Aliendelea na kazi nilivyokuwa Rais nilimteua, nilimwita nikamwambia nataka nikuteue akasema nakushukuru sana kaka, nikamwambia naamini utaiweza akasema sina wasiwasi nitaimudu tu,” alisema jana kwenye maziko yake Mvumi wilayani Chamwino, mkoani Dodoma na kuongeza:


“Kwa kweli amefanya kazi nzuri iliyotukuka, nakumbuka katika kipindi cha wimbi la kikombe cha Babu wa Loliondo alikuwa Mkurugenzi wa NIMR, watu wanakwenda, wanatoa wagonjwa hospitalini hata kwenye Baraza la Mawaziri niliona wanakunywa.”

“Tulipitia kipindi kile kigumu vizuri alitushauri serikali, santuri ikaisha ugumu wake (kikombe), baadaye alipata kazi WHO Afrika na baadaye Makao Makuu…nilikutana na Mkurugenzi wa WHO namuuliza dada yangu anaendeleaje akaniambia ndiyo mkono wangu,” alisema.

Kikwete alisema “Mzee John Malecela umepoteza mtoto, familia imepoteza mwanafamilia muhimu, mimi nimepoteza dada maana kila tukikutana namwita dada, rafiki, lakini taifa limepoteza mmoja wa raia wema, wazalendo wa kweli.
Mwele ameondoka siyo rahisi kuamini kama hatunaye, hatutamwona na hatutakutana tena.”


Alisema taifa litamkumbuka kwa mema mengi aliyoifanyia nchi na dunia kwa ujumla.

“Rais Mwinyi alikuwa anapenda kusema unataka historia yako iandikwaje nafikiri historia ya Dk. Mwele imeandikwa vizuri sana hivyo tunatakiwa kuungana kwa pamoja na familia kumwombea mapumziko mema na mzee tunakupa pole sana kwa msiba huu mzito,” alisema Kikwete.

Aidha, Kikwete aliongoza viongozi wa serikali na mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa katika maziko.

Kikwete aliwasili katika kijiji cha Mvumi nyumbani kwa Waziri Mkuu mstaafu, Mzee John Samwel Malecela, majira ya saa 9:30 alasiri akiwa amefutana na mkewe Salma Kikwete na kupokelewa na viongozi wengine akiwamo Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya tatu, Fredrick Sumaye na wawakilishi kutoka (WHO).


Awali, katika ibada ya kuaga mwili wa Dk. Mwele, iliyofanyika katika Kanisa la Aglikana Dayosisi ya Kati, Askofu wa Kanisa hilo Dk. Dickson Chilongani, alisema hakuna msiba unaouma sana kama kuondokewa na mtoto wa kumzaa.

“Sote tunategemea sana kutangulia kabla ya watoto wetu, lakini Mungu ndiye amepanga na ikitokea hivyo hakuna anayeweza kuvumilia maumivu yake, maneno ya kibinadamu hayawezi kuondoa maumivu yenu Mungu ndiye pekee atakaye ondoa maumivu hayo.

“Dk. Mwele alikuwa na mchango mkubwa sana kitaifa na kimataifa tulitamani aendelee kuwapo ameondoka mapema sana wakati ambao bado tulikuwa tunahitaji kunufaika na matunda yake jambo la muhimu ni sisi kuendelea kuenzi mema yake aliyofanya katika wakati wa uhai wake,”alisema Askofu Dk. Chilongani.

Sumaye alisema: “Napenda kuungana nanyi katika msiba huu …nitamkumbuka sana kwa jambo moja ambalo ni misimamo yake aliyokuwa nayo katika mambo ambayo yeye alikuwa anaamini hakuwa mtu wa kuyumbishwa na mtu katika kile anachokiamini.”


Aidha, alisema Tanzania imempoteza mtu ambaye matunda yake yalikuwa bado yanahitajika kitaifa na kimataifa na taifa litaendelea kujivunia kazi aliyoifanya ndani na nje ya mipaka yake.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum Ikulu), George Mkuchika, alisema Dk. Mwele, alikuwa ni mcha Mungu.

“Mara nyingi tulikuwa tunakutana na Dk. Mwele baada ya kutoka kwenye ibada alikuwa anapenda sana kujiombea mwenyewe ndiyo maana hata leo hii sisi tunamwombea ni kazi sana kumwombea mtu ambaye alikuwa haombi wakati wa uhai wake,” alisema Mkuchika katika maziko hayo yaliyohudhuriwa na umati.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad