Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro ameagiza kufunguliwa kwa jalada la uchunguzi la vijana watano wanaodaiwa kutoonekana tangu Desemba 26 mwaka jana katika maeneo ya Kariakoo ‘Kamata’ jijini Dar es Salaam.
IGP Sirro alitoa kauli hiyo jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi ambapo alikiri kupata taarifa za tukio hilo na
“Hilo nilielezwa lakini niliwaambia wafungue jalada la uchunguzi ili tufuatilie kwa hiyo Makao makuu wanafuatilia suala hilo ili tuweze kujua kuna nini,”alisema IGP Sirro baada ya kuulizwa hatima ya vijana hao na familia zao.
Baada ya kupotea vijana hao, ndugu zao walianza kufuatilia huku wakidai hawapati msaada unaostahili kutoka kwa Jeshi la Polisi tangu walipotoa taarifa ya jambo hilo Desemba 27, 2021. Waliopotea ni Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe.
Sylvia Quentin, Mama mzazi wa Tawfiq Mohamed alisema siku ya mwisho mmoja wao alituma ujumbe mfupi wa simu (sms) kuwa wamekamatwa eneo la Kariakoo wakiwa kwenye gari aina ya Toyota IST nyeusi na wanapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo ndugu hao walianza kuwafuatilia, ikiwamo kuzunguka kwenye vituo vingine vya polisi bila mafanikio, ndipo walianza kuzungukia kwenye hospitali mbalimbali katika vyumba vya kuhifadhia maiti hata hivyo hawajawapata ndugu zao.
Saa 48 vituoni
Kuhusu malalamiko ya watu kushikiliwa katika vituo vya polisi kwa zaidi ya saa 48 bila kufikishwa mahakamani, IGP Sirro alisema “Kuna makosa ambayo sheria hiyo ya saa 48 haiwezi kutumika, mfano tuhuma za ugaidi, mauaji na nyinginezo,”alisema na kufafanua
“Lakini wakati mwingine changamoto unakuta mtu ametoka Musoma hapa hana ndugu unamkamata. Kesi labda ni utoaji wa lugha chafu, huyo mtu unamuachiaje, hana mtu wa kumdhamini, kwa hiyo inatokea mara moja moja kwa sababu kila baada ya saa sita tunatakiwa kukagua mahabusu.”
“Kwa hiyo kama mtu anaweza kupewa dhamana halafu amekaa zaidi ya saa 48, basi ni uzembe wa watendaji, tupate taarifa tu ili tuweze kuwashughulikia maofisa hao.”
Alisema kuwa baadhi ya waathirika wa tuhuma fulani kukosa uvumilivu baada ya mtuhumiwa kuachiwa kwa dhamana.