Jamhuri "Sabaya Alitumia Silaha Kupora"



WAKILI wa wajibu rufani kwenye kesi ya jinai namba 105, Ofmedy Mtenga, amedai mahakamani kuwa silaha zilitumika katika tukio la kupora fedha na mali nyingine katika tukio linalodaiwa kufanywa na Lengai Ole Sabaya kwenye duka la Mohamed Saad, lililoko Mtaa wa Bondeni jijini Arusha.

Wakili huyo alitoa madai hayo jana wakati wa usikilizwaji wa Rufani namba 129, katika shauri lililokuwa linamkabili, Ole Sabaya na wenzake wawili, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sedekia Kisanya.

Akijibu hoja ya saba ya mawakili wa waleta kwa nini wateja wao walistahili kutiwa hatiani na kufungwa miaka 30 kwenda jela, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mtenga, alidai kwamba kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na mashahidi wa mashtaka katika tukio hilo kulikuwapo na silaha.

Alidai kwamba kwa mujibu wa shahidi wa sita wa mashtaka Bakari Msangi, kwenye kielelezo cha kwanza walichokitoa mahakamani cha maelezo aliyoandika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, silaha zinaonekana kutumika katika tukio la kupora mali na kuwaweka watu chini ya ulinzi.

"Ushahidi unaonyesha kuwa kulikuwapo na watu wengi siyo rahisi kwa kila mtu kuona kila kitu kinachoendelea kwa kuwa kila mmoja alikuwa amewekwa kwenye sehemu yake, pia siyo kila mmoja atakuwa jasiri wa kuangalia tukio linavyoendelea.”


"Mazingira ya tukio yalikuwa mabaya sana hivyo kwa mashahidi kujichanganya kwenye maelezo yao, ni kutokana na wao kuwa sehemu tofauti na wengine wakiwa wamelazwa kifudifudi na kufungwa pingu, Wakili Mtenga,"alidai.

Naye Wakili wa Serikali, Veridiana Mlenza, alipinga hoja ya kwamba aliyeandikwa kwenye hati ya mashtaka, Mohamed Saad ni tofauti na yule aliyekwenda mahakamani kutoa ushahidi, Mohamed Saad Hajirini.

"Jaji hoja yao haina mashiko kilichotokea ni kwamba katika hati ya mashtaka yalitumika majina mawili na shahidi alipokuja hapa mahakamani alijitambulisha kwa majina matatu hivyo hakuna utofauti wa majina kama walivyodai kwa kuwa eneo ni sahihi na halina utata wowote," alidai Mlenza.


Alidai ya kuwapo kwa mkanganyiko eneo la tukio lilipotokea na duka lilipo haina msingi kwa kuwa ni sehemu sahihi na waleta rufani awali walikaa kimya.

Naye Wakili Mwandamizi, Baraka Mgaya, alidai kuhusu kufanya marekebisho ya hati ya mashtaka kwa kuwa kuna vitu ambavyo havikuorodheshwa, ikiwamo waleti kwenye eneo hilo, aliwezi kuathiri chochote kwa kuwa shahidi wa sita wa mashtaka, Bakari Msangi, alikana kuwapo na pochi siku ya tukio.

Aliieleza Mahakama kwamba kwa mujibu wa shtaka la tatu, fedha na simu aina ya Tekno Pop 1 ziliorodheshwa katika hati ya mashtaka isipokuwa karatasi ya mahitaji, ambayo waliona haina thamani na wasingeweza kuthibitisha mahakamani.

"Kushindwa kuthibitisha kitu kimoja haiwezi kufuta kabisa shtaka hilo na katika shtaka la kwanza kuna vitu viwili viliongezeka vikiwamo fedha za sarafu na mashine ya kielekroniki na kwa mujibu shahidi wa pili washtaka, alidai kwamba hakufahamu kiasi hali cha sarafu, lakini kwa suala la EFD ni mali na ombi letu wakati Mahakama yako ikitoa uamuzi iangalie kwa kosa la kwanza kutokuwekwa kwa mashine hiyo, je, iliwaathiri nini waleta rufani?”


Wakili Mlenza alidai kwamba hati hiyo siyo batili na imekidhi vigezo vya kisheria na warufani walifahamu ni makosa gani yanawakabili.

Vile vile, Wakili Mtenga alidai hakuna utata katika suala la utambuzi wa mleta rufani wa tatu, Daniel Mbura, kwa kuwa awali alimtambua baada ya Sabaya kumwita kwa jina lake wakiwa dukani kwa Mohamed Saad na polisi baada ya kufanyika kwa gwaride la utambuzi na polisi nao walimjulisha jina halisi la mkata rufani huyo.

Kuhusu maelezo aliyoandika, Bakari Msangi, kituo cha polisi na kutofautiana na ushahidi ulioutoa mahakamani kwa kuwa kulikuwapo na ushawishi wa kumshawishi kutokuendelea na kesi uliofanywa na askari wa polisi Kalebu, pia hawakumsomea maelezo baada ya kuandika maelezo hayo.

Kadhalika, kuhusu hoja ya mashahidi wa pili na nne kupewa dhamana na polisi na akiwamo, Deogratius, anayesemekana alipewa dhamana na alitakiwa kuunganishwa katika shauri hilo, alidai kwamba tukio lililoripotiwa awali lilikuwa shambulio la kudhuru na siyo unyang’anyi wa kutumia silaha na Deogratius alivunja dhamana.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad