KARIBU shule zote za umma za msingi na sekondari zinaelezwa kuwa zina uhaba wa walimu, hali hiyo inaathari, kwa sababu inasababisha wanafunzi kutofundishwa kikamilifu masomo kwa mujibu wa mtaala.
Kwa hiyo kuwaongozea gharama zaidi wazazi na walezi, kutafuta masomo ya ziada kwa watoto wao yakiwamo yale yasiyofundishwa.
Shule za sekondari ndizo zenye uhaba huo wa walimu wa kutisha, hali ambayo ni vyema ikatafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi, lakini kupata wataalamu wa fani mbalimbali wa baadaye.
Uhaba huo wa walimu unazikumbuka shule nyingi, lakini Sekondari ya Kenswa iliyoko Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi, ni miongoni mwa shule zenye tatizo hilo.
Taarifa zinasema walimu wanaohitajika ni 29, lakini walioko ni 10 pekee hali inayosababisha waelemewe na mzigo mkubwa wa kufundisha.
Shule nyingine yenye tatizo kama hilo, ni Magema Sekondari iliyoko Wilaya ya Geita mkoani Geita, ambayo imewahi kuripotiwa na ITV kuwa ina walimu wawili, katika taarifa ITV shule hiyo ilikuwa na walimu wawili, huku idadi kubwa ya wanafunzi wakikosa kufundishwa masomo mengine yakiwamo ya sayansi.
Hivyo baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wanaiambia ITV na kuiomba serikali kuwaongezea walimu, kwa kuwa wawili waliokuwapo walikuwa hawatoshi kufundisha masomo yote, ni janga shule kuwa na walimu wa wawili, ukweli ni kwamba, si rahisi kufundisha wanafunzi masomo yote na badala yake wazazi na walezi itabidi wanalazimike kulipia watoto wao gharama za twisheni.
Uhaba huo unasababisha watafute walimu wa kuwafundisha watoto wao masomo wanayoyakosa shuleni, kwani mitihani ni wa masomo yote, bila kujali kwamba mengine hawajafundishwa.
Kwa hali kama hiyo ni wazi inabidi wazame zaidi mifukoni kutoa pesa ili kulipia masomo ambayo hayana walimu shuleni, hali ambayo ni wazi wanajikuta wakipata gharama ambazo wakati mwingine ziko nje ya bajeti.
Miongoni mwa masomo ambayo mara nyingi huwa hayana walimu ni ya sayansi kuanzia kemia, fizikia na baiolojia ambayo kwenye twishen' hutozwa kuanzia Shilingi 25,000 kwa somo moja.
Ninatambua kile ambacho serikali inakisema kuwa, inaendelea kupunguza uhaba wa walimu katika shule zake ili kukabiliana na upungufu wa watumishi nchini kadri ya mahitaji yatakavyojitokeza hasa walimu wa sayansi.
Inakiri kwamba, kwa nchi nzima uhaba wa walimu upo hasa kwa walimu wa sayansi, ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, anasema serikali itaendelea kutoa ajira hasa za walimu wa sayansi ili kupunguza upungufu huo wa walimu. Lakini swali linabaki tutangojea mpaka lini?
Ingekuwa ni vyema kama kasi ya kuajiri walimu wa masomo hayo, ikaongezeka ili kupunguzia wazazi gharama za twisheni, lakini kuandaa wataalamu wa kutosha wa fani mbalimbali hapo baadaye.
Ingependeza juhudi ambazo zimetumika kujenga madarasa na kuwafanya wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu kwa pamoja, zingetumika pia kuhakikisha shule zinakuwa na walimu wa kutosha ili kukabiliana na upungufu huo unaoathiri elimu.