Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Jerry Muro amewataka wasemaji wa klabu ya Young Africans kusoma alama za nyakati na sio kukurupuka na kuzungumza na Waandishi wa Habari.
Jerry Muro ambaye aliwahi kuwa Afisa habari wa Young Africans ametoa ushauri huo kwa wasemaji wa klabu hiyo kwa sasa, ikiwa ni saa kadhaa baada ya kufanyika kwa mkutano na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya klabu hiyo leo Jumanne (Februari 08), Jijini Dar es salaam.
Mkutano huo na Wanahabari umefanywa chini ya Afisa Habari wa klabu hiyo kwa sasa Hassan Bumbuli na Msemaji wake Haji Sunday Manara, huku ajenda kuu ikiwa ni kutoridhishwa na mwenendo wa baadhi ya waamuzi waliochezesha michezo yao msimu huu.
Ajenda nyingine katika mkutano huo ilikua ni kulitaka shirikisho la soka nchini TFF kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi wa klabu na wadau wengine kama inavyofanya kwa baadhi wa viongozi wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Jerry Muro amesema: “Inashangaza kumsikia Afisa Habari wa klabu akielezea baadhi ya mambo ya msingi ya timu kama shabiki au kuongelea masuala ya ufundi kama kocha wakati kazi hizo si zao.”
“Hata kama klabu zina utaratibu wa kuwapa fursa ya kuzungumza na kutoa ufafanuzi wa mambo yanayoulizwa na waandishi wa habari, lakini wamekuwa wakienda mbali na mipaka yao.
“Ifike wakati wasemaji wa Yanga waonyeshe ukomavu katika kazi wanazopewa, wasikurupuke na kuonekana vituko.”
Kwa hali hiyo ni dhahir Jerry Muro hajafurahishwa wala kuyapokea yaliyozungumzwa katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Makao Makuu ya klabu ya Young Africans leo Jumanne (Februari 08) jijini Dar es salaam