JICHO LA MWEWE: Ebu kutana na 'Mfanyabiashara' maarufu Morrison



KUTANA na Mfanyabiashara maarufu kutoka nchini Ghana. Jina? Bernard Morrison. Sehemu ya kuzaliwa? Mankessim, Ghana. Umri? Miaka 28. Urefu? Futi 5 inchi 10. Anaishi maeneo mbalimbali katika jiji la Dar es Salaam.

Kama ulidhani Bernard Morrison ni mchezaji mahiri ulikosea. Ni mfanyabiashara mahiri pengine kuliko unavyodhani kwamba ni mchezaji mahiri. Amekuja nchini akatusoma na anajua anachofanya. Licha ya kwamba ni mchezaji mahiri, pia ni mtu mwenye akili nyingi pengine kuliko wengi ambavyo wanadhani.

Inawezekana hakuja na akili zake timamu wakati Yanga walipomtoa kijijini kwao Ghana. Lakini alipofika Dar es Salaam akaamua kutumia akili zake timamu. Mifano ipo mingi ya namna ambavyo Morrison aliamua kutumia akili zake timamu pindi alipofika Dar es Salaam.

Alichungulia kwa umakini namna ambavyo watani wa Yanga na Simba walivyo mambo safi. Kila kitu kilikuwa mambo safi ndani na nje ya uwanja. Ndani ya uwanja Simba walikuwa timu bora. Nje ya uwanja Simba walikuwa na maisha bora. Katika msimu wake wa kwanza Yanga, ndio kwanza GSM walikuwa wameingia lakini walikuwa hawajajipanga vema.


 
Msimu huo Yanga walikuwa wamesajili wachezaji butu. Usimsahau pia Yikpe. Lakini pia GSM walikuwa hawajawekeza vya kutosha nje ya uwanja. Kambi ya Yanga ilikuwa ya kawaida tu katika hoteli moja ya kawaida pale maeneo ya Mikocheni. Simba walikuwa wanaishi kwa raha kando ya ufukwe maeneo ya Mbezi Beach.

Morrison alichungulia na kuamua kujiuza kimya kimya. Alijua alichofanya. Akaiuza bidhaa yake adimu ambayo ni miguu yake. Aliupiga vema mpira akiamini kwamba alikuwa anajitengenezea soko nchini. Na kweli. Simba wakaanza kumnyemelea kimya kimya. Kwake ilikuwa fursa.

Mwisho wa msimu, licha ya matatizo yake ya mkataba na waajiri wake wa zamani lakini akafanikiwa kusaini Simba. Pesa ilikuwa nono kwa sababu wakati anakaribia kuondoka Yanga, yeye ndiye alikuwa mchezaji muhimu zaidi klabuni. Kama kuna kitu kiliwaumiza Yanga ni Morrison kuondoka. Subiri kwanza, sio kuondoka, bali kuondoka na kwenda Simba.


Baada ya kusaga chumvi katika kidonda cha Yanga, Morrison hatimaye alitua Simba kwa pesa ndefu, lakini pia mwishowe alishinda kesi ya kimkataba ambayo Yanga walikuwa wameipeleka pale Zurich wakidai uhalali wa mchezaji wao.

Tatizo ni kwamba, licha kujikuta akicheza Simba muda mwingi alijikuta katika sakata lenyewe, lakini zaidi kuliko kutumikia mkataba. Kwa muda mrefu Simba walijikuta katika shauku ya kusubiri tamati ya sakata lake, lakini ghafla wakajikuta wapo mwisho mwisho wa mkataba wa mchezaji mwenyewe.

Kifupi ni kwamba sakata la Bernard lilidumu sana Simba kuliko mashabiki wa pande zote mbili kuzingatia kazi yake. Ilikuwa hasara kwa Simba ambapo ghafla Bernard alijikuta akimaliza utata wa mkataba wake, huku akiwa amekaribia kumaliza mkataba husika.

Na sasa Morrison amebakiza miezi minne tu ya mkataba wake Msimbazi. Ijumaa jioni Simba wametangaza kumsimamisha kwa muda usiojulikana. Habari za ndani kabisa ni kwamba Morrison amekutwa na matatizo yale yale ambayo alikuwa anayafanya katika siku zake za mwisho Yanga.


 
Usidhani kama ni bahati mbaya. Morrison amechungulia vitu vingi. Amechungulia kwamba kwa sasa kuna timu mbili ambazo zinaweza kumpa pesa nyingi pengine kuliko zile ambazo Simba wanaweza kumpa kama akisaini mkataba mpya. Ana akili nyingi. Kuna Yanga na Azam.

Tuiweke kando kidogo Azam. Twende na Yanga. Kile kile ambacho kilimpeleka Simba wakati ule ndicho ambacho kinaweza kupatikana Yanga kwa sasa. Maisha safi ndani na nje ya uwanja. Yanga ya leo sio ile ambayo Morrison aliiacha. Hii imeimarika.

Nje ya uwanja wameondoka katika ile hoteli ya Mikocheni na sasa na wanaishi kambi ya kifahari kule Kigamboni. Ndani ya uwanja wanaongoza kwa tofauti ya pointi nyingi dhidi ya Simba na wala hawajabahatisha. Wanacheza soka maridadi. Wamekusanya mastaa. Wanaimbwa kila kona na mashabiki wao wamerudi tena viwanjani.

Nahofia kwamba vituko vyote hivi ambavyo Morrison anawafanyia Simba ni kwa sababu anajiweka sokoni wakati huu mkataba wake ukiwa unakaribia kukata roho pale Msimbazi. Ana akili nyingi. Sina uhakika kama ana mawasiliano na waajiri wake wa zamani au klabu nyingine ndani na nje ya nchi.


Ninachojua ni kwamba anajaribu kufanya biashara yake ya miguu hasa katika nchi hii ambayo viongozi wa mpira na mashabiki wake huwa hawaguswi sana na matatizo ya kinidhamu ya mchezaji wa timu pinzani na zaidi wanajikita katika kukomoana.

Kwa mfano, wakati ule Yanga walipokuwa wakilalamika kwamba Morrison alikuwa mtovu wa nidhamu nilikutana na kiongozi mmoja wa Simba ninayemuheshimu sana alidai kwamba watu wa Yanga walikuwa wanamuonea sana Morrison. Hakusikiliza madai ya Yanga kwa sababu tayari walikuwa na uhakika wa kumpata Morrison.

Yale yale ambayo inadaiwa kwamba Morrison alikuwa anayafanya Yanga ndio ambayo kwa sasa Simba wanamtuhumu nayo. Natamani kukutana na kiongozi yule na kupata maoni yake kama kweli Yanga walikuwa wanamuonea wakati ule. Huenda akawa amebadilisha mawazo yake.

Mwisho wa siku Morrison hajali sana. Yeye ni Mghana na ni mfanyabiashara mzuri tu. Tatizo tunajaribu kumpa timu. Tunajaribu kumpa mapenzi na timu zetu kitu ambacho yeye hana. Kwa upande huu napenda kumpongeza kwa sababu anawafundisha vijana wetu jinsi ya kuwa wachumi wazuri wakati wanacheza soka.

Nawajua wachezaji wengi ambao wanakufa maskini kwa sababu ya kujifanya ni mashabiki wa timu hizi. Morrison anajaribu kutufundisha namna ya kuwa wafanyabiashara katika kazi hii. Unaweza kumchukia au kumpenda lakini yeye anazungumza na akaunti yake ya benki.


 
Amejua jinsi gani ambavyo tunaishi katika soka la kukomoana kuliko kujali weledi.

Tuone itakuwa vipi mwisho wa safari yake Msimbazi, lakini sidhani kama atavaa jezi nyekundu na nyeupe msimu ujao.

Kitu ambacho sifahamu ni kama atabakia nchini. Lakini kitu ambacho sifahamu zaidi ni kwamba akibaki nchini atabakia timu gani
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad