JICHO LA MWEWE: Kichekesho mikataba ya Mwamnyeto na Onyango



KWAMBA mabeki wawili mahiri wa Simba na Yanga, Joash Onyango na Bakari Mwamnyeto mikataba yao inakaribia ‘kukata roho’ mwishoni mwa msimu huu na haionekani kuwa habari kubwa sana kwa viongozi, mashabiki na vyombo vya habari nchini. Ulaya ingeweza kuwa habari kubwa.

Onyango na Mwamnyeto, ni mabeki mahiri kama walivyo, hauwezi kudhani ndani ya miezi mitatu tu mikataba yao inafika mwisho. Klabu zao hazina wasiwasi. Kuna sababu kubwa inayochekesha ndani yake. Hauwezi kuiona kwa nje. Watani hawajakabiliana pabaya kama ilivyo kawaida yao.

Kila mmoja hana wasiwasi na wizi wa mwenzake. Nadhani Simba wanaamini Yanga hawana haja sana na Onyango. Kisa? Yanga ina mabeki wawili mahiri kwa sasa. Mwamnyeto na Dickson Job aliyeondokea kuwa kipenzi cha Wanayanga kama ilivyo kwa Mwamnyeto.

Zaidi ya hilo, Yanga wana Yannick Bangala ambaye licha ya kuwa kiungo mahiri, lakini ana uwezo mkubwa wa kurudi nyuma zaidi na kucheza kama beki wa kati. Amekuwa akifanya hivyo mara nyingi. Simba hawawezi kuumiza kichwa sana kuvamiwa kwa Onyango.


 
Inavyoonekana Yanga nao hawana wasiwasi na wizi kutoka kwa wapinzani wao. Kisa? Wanaamini wapinzani wao wametulia kwa mastaa wao wawili wa kati. Onyango na Henock Inonga. Hii ni hadithi ya kila mtu abaki na mchezaji wake. Hakuna kuibiana.

Jaribu kufikiri namna ambavyo Yanga walienda kasi na Mwamnyeto wakati akiwa na Coastal Union. Ni kwa sababu Simba pia walikuwa wanamtaka mlinzi huyo mahiri wa timu ya taifa. Wakati huo wote walikuwa wanasaka walinzi wa kati. Bila ule upinzani hali ingekuwa kama sasa. Mwamnyeto alipata dili zuri.

Pia inaonekana kama vile wachezaji wenyewe huenda wasitake rabsha ya kuhatarisha nafasi zao wakijaribu kuhamia kwingine. Kwa mfano, Mwamnyeto anaweza kuuvunja ukuta wa Inonga na Onyango na kisha akacheza na mmoja kati yao? Nani angependa kujihatarisha kukaa benchi bila ya sababu.


Lakini inawezekana hali ya hewa imetulia kwa sababu nafasi wanazocheza wachezaji huwa hawabadiliki mara kwa mara. Kuanzia kwa kipa hadi walinzi wa kati, kama timu imetulia ni nadra sana kuletewa wapinzani wa kweli.

Kuna nafasi ambazo wakubwa huwa zinawasumbua na maongezi yangekuwa mengi nyakati hizi katika vyombo vya habari. Mfano namna ambavyo Clatous Chama alipokuwa akielekea katika siku za mwisho za mkataba wake Msimbazi. Hali ilikuwa tete. Kisa? Yanga hawakuwa na mchezaji wa aina yake.

Sio kwamba hawakuwa na mchezaji wa aina yake lakini pia hawakuridhika na wachezaji wa nafasi yake katika timu yao. Kelele zilikuwa nyingi na mpaka Simba walipohaha kumbakisha kwa mkataba mpya walikuwa wamechoka kweli kweli. Mithili ya mwanadamu aliyekimbilia kilomita 42.

Kama unabisha katika hili jaribu kufikiria kama mkataba wa Fiston Mayele ungekuwa umebakiza miezi mitatu kama huu wa Mwamnyeto. Jinsi ambavyo washambuliaji wa Simba hawapo katika fomu basi jasho lingewatoka mabosi wa Jangwani. Tungesoma tu vichwa vya habari ‘Mayele amalizana na Simba’.


 
Ni simulizi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Shomari Kapombe. Yanga walikuwa hawajatulia katika nafasi zao na tuliona kasheshe nzito kuelekea miezi michache ya mwisho ya mikataba yao. Ni tofauti na hali ilivyo sasa kwa Onyango na Mwamnyeto. Viongozi wamejikuta wakipumua zaidi.

Nadhani ipo pia kwa Shomari Kibwana na Yassin Mustapha. Yanga hawana wasiwasi sana kwa sababu wanajua Simba ina Kapombe na Tshabalala ambao wana mikataba mipya klabuni hapo. Vinginevyo wangekuwa wanakimbizana mida hii.

Kwa Onyango na Mwamnyeto pia kuna jambo jingine nyuma ya pazia. Achilia mbali wachezaji wenyewe kutotamaniwa na wapinzani lakini kuna ukweli wachezaji wenyewe hawatazami fursa nje ya mipaka ya Tanzania. Wameridhika na walipo.

Onyango katika umri wa miaka 29 inaonekana Tanzania amefika mwisho. Tukumbuke kwanza kwa yeye kuwa Simba ni anacheza timu ya ugenini. Kwao ni Kenya na hauwezi kumlaumu kutosogea kwingine kwa sababu tayari analipwa pesa nyingi kuliko klabu za Kenya ambavyo zingemudu kumlipa.


Mwamnyeto kama ilivyo kwa mastaa wetu, inaonekana wazo hilo halipo. Vinginevyo hizi zilikuwa nyakati za kuondoka katika klabu zetu kiulaini zaidi.

Klabu zetu zinaweza kukugeuza mfungwa kama una mkataba. Unapomaliza mkataba inakuwa fursa nzuri.

Kwa wachezaji wetu kama hakutakuwa na ujanja wa ziada kutoka kwa watani au Azam basi unalazimika kuendelea kuwepo. Hakuna soko jingine nje ya hapo. Ni wachezaji wachache wanaoweza kutazama soko jingine nje ya hapo na kutumia kile kinachoitwa Bosman Rule.

Kwa klabu inakuwa nafuu. Ni nyakati ambazo hawajuti kumpa mchezaji mkataba mfupi. Mkataba wa miaka miwili ni kosa kubwa la kiufundi, lakini hauwezi kuligundua kosa lenyewe kama unajiweka katika nafasi ya kuendelea kumbakisha Mwamnyeto kiulaini.

Labda tungehitaji soko jingine kubwa la ndani kwa wachezaji wetu mahiri. Vinginevyo sio kitu cha faida sana kwa kina Onyango. Jaribu kuangalia nchi nyingine zilizoendelea kisoka ambazo pia zina uchumi mkubwa.


 
Waingereza wana Chelsea, Man City, Manchester United, Arsenal na Liverpool. Sasa wameongezeka Newcastle United. Wote hawa wanakidhi matakwa ya mastaa wao

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad