IJUMAA iliyopita amefariki dunia beki wa Ruvu Shooting, Ally Mtoni ‘Sonso’ na alizikwa Jumamosi. Sonso enzi za uhai wake aliwahi pia kuzicheza Lipuli, Yanga na Kagera Sugar. Zaidi ya hapo amewahi kuipigania jezi ya timu ya taifa.
Ni mara chache kwa taifa letu kutokea kifo cha mchezaji wa Ligi Kuu ambaye anaendelea kucheza soka. Tumewahi kushuhudia wachezaji wengi wa zamani walioacha soka wakifariki lakini sio kwa wachezaji ambao wanaendelea kucheza.
Jina lake lipo katika ofisi za TFF kama mchezaji wa Ligi Kuu na ni Novemba mwaka jana tu Sonso alikuwa amecheza pambano lake la mwisho la Ligi Kuu. Ni Novemba mwaka jana tu tunaambiwa kwamba Sonso alishapangwa katika kikosi ambacho kingecheza na Simba, lakini mguu ukaanza kumpa maumivu.
Huu ulikuwa mwanzo wa safari yake ya mwisho. Kinachosemwa ni kwamba baada ya hapo alipelekwa hospitali ya Muhimbili lakini yeye na familia yake wakamtoa hospitali na kuamua kumpeleka kusikojulikana kwa ajili ya matibabu zaidi.
Hili ni fumbo. Kusikojulikana ni wapi? Hatuwezi kufichana kuhusu matibabu. Sonso alikwenda kupata matibabu ya kienyeji. Inadaiwa kulikuwa na hisia kwamba huenda alikuwa amefanyiwa mambo ya kishirikina. Sio jambo jema.
Kumekuwa na wimbi la wachezaji ambao wanaamua kuifuata njia hii. Hatuelewi kwanini, lakini kikubwa zaidi ni elimu miongoni mwa wachezaji wetu. Wachezaji wetu wanapaswa kufundishwa kuamini katika magonjwa halisi yaliyopo na yanayoweza kutibika kitalaamu.
Staa mmoja wa Yanga aliwahi kupata hisia hizi. Akagomea matibabu ya hospitali. Alikwenda kusikojulikana kwa ajili ya kupata matibabu, lakini hali ikaendelea kuwa mbaya. Baadaye Yanga wakamkimbiza Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu zaidi. Alirudi akiwa ametengemaa na maisha yake ya soka yanaendelea. Alitibiwa kitaalamu zaidi kwa mujibu wa ugonjwa wake na hali ikawa sawa.
Imewahi pia kutokea hapo zamani kwa staa wa zamani wa Simba na timu ya taifa. Aliwahi kupata majeraha ya kawaida, lakini akagoma kutibiwa katika njia za kawaida za kitabibu. Bahati mbaya alikuwa anaelekea katika siku zakeza mwisho za maisha yake ya soka. Sijui kama alienda hospitalini au vinginevyo. Namuona akicheza mechi za mitaani.
Hili ni fundisho kwa soka letu na tunahitaji kujitafakari. Tunahitaji elimu kwa wachezaji wetu. Elimu ya saikolojia na elimu ya kawaida kabisa. Itasaidia kwa wachezaji kujua kwamba mwanadamu, hasa mwanamichezo anaweza kuumia kama Cristiano Ronaldo huwa anaumia.
Unajaribu kujiuliza kwa Sonso. Ni kwanini ilifikirika hivyo? Timu kama Ruvu Shooting ina riziki gani ya kuweza kuwahangaisha wachezaji wawafanyie wachezaji wenzao mambo mabaya? Kama haikuwa hivyo Yanga vipi itokee kwa Ruvu Shooting?
Kitu kingine ambacho kinaweza kuwahangaisha wachezaji wetu ni bima ya Afya. Wachezaji wetu wana bima za Afya? Tufanye kwamba Sonso angeamua kukaa hospitalini na matibabu yake yakachukua muda mrefu. Je ni kweli alikuwa na bima ya afya?
Wachezaji wengi wa Ligi Kuu hawana bima za Afya. Sio kwa wao tu, bali pia kwa familia zao. Mchezo wa soka unaonekana kama sehemu ya kuzugia tu na sio kazi kamili. Ni kosa kubwa kwa mwanamichezo kukosa bima ya Afya hasa ukizingatia pia kazi zao zinawafanya wawe katika hatari kubwa ya kuumia.
Wengine wanaweza wasiumie kazini, lakini mtazame mchezaji kama Gerald Mdamu wa Polisi Tanzania ambaye aliumia katika ajali ya gari akiwa na timu. Baadaye ilibainika kwamba Mdamu hakuwa na bima ya Afya. Hata kama angeumia ndani ya uwanja bado angepata wakati mgumu.
Wachezaji wa Yanga, Simba na Azam wana bahati ya kwenda kutibiwa nchi za nje. Wapo wanaokwenda zaidi Afrika Kusini lakini Yanga pia wameanzisha utaratibu kwa kuwapeleka wachezaji wao Tunisia. Sio kila timu inaweza kufanya hivi. Tusisitize wachezaji kuwa na bima. Mchezaji anayefikia hadhi ya kucheza daraja la pili, la kwanza na Ligi Kuu lazima awe na bima.
Tukirudi kwa Sonso, ndani ya uwanja nitafafanua mambo mawili. Kwanza kabisa tumempoteza mchezaji ambaye alikuwa na umbo refu kabla ya kila kitu. Baada ya maumbo ya kina Bakari Malima kuondoka nchini kwa sasa tumebakiwa na wachezaji wachache warefu hasa katika maeneo ya ulinzi. Sonso alikuwa mmoja wao.
Lakini vile vile tumempoteza mchezaji aliyeweza kucheza nafasi nyingi tofauti uwanjani. Angeweza kucheza kama beki wa kushoto, pia kama beki wa kati na pia alimudu kiungo cha ukabaji yaani namba 6. Hii pengine ilitokana na matumizi sahihi ya mguu wake wa kushoto.
Hatuna wachezaji wengi wanaoweza kufanya hivi katika zama za kisasa. Wengi wanaweza kucheza nafasi moja uwanjani. Kitu ambacho kwa sasa Dickson Job au Kibwana Shomari wamekuwa wakiifanyia Yanga ni kitu adimu kwa soka letu.
Zamani tulikuwa na wachezaji wengi ambao wangeweza kucheza katika nafasi tofauti kutokana na upungufu wa baadhi ya wachezaji uwanjani. Marehemu Saidi Mwamba Kizota alikuwa mmojawao. Angeweza kucheza nafasi tatu uwanjani. Angeweza kucheza kama beki wa kati, kiungo na pia mshambuliaji. Mungu amrehemu.
Pamoja na yote haya, lakini kifo cha Sonso kimetukumbusha umoja wetu katika soka. Inawezekana Sonso hakuwa maarufu sana kama Mbwana Samatta, lakini jamii ya wanamichezo imewakumbusha watu wa fani nyingine jinsi mchezo wa soka ulivyo na nguvu.
Msiba wa Sonso ulitufanya tuwe wamoja na kuungana katika majonzi yetu. Ambao wapo katika fani nyingine na hawakumfahamu Sonso walijikuta wakimfahamu na kutaka kujua mengi yanayomuhusu. Ni heshima pia kwa familia yake.
Mungu amlaze mahala pema peponi.