KAKA wa mke wa mfanyabiashara ya madini bilionea Erasto Msuya, Mbazi Mrita ameieleza mahakama alivyomtafuta dada yake, Miriam Mrita bila mafanikio hadi alipomkuta mikononi mwa polisi siku 10 baadaye.
Mrita ni mfanyakazi katika hoteli ya SG Northern Adventures inayomilikiwa na dada yake, Miriam.
Jana alitoa madai hayo alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ya mauaji inayomkabili dada yake katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Mbele ya Jaji Edwin Kakolaki, Mrita alidai sakata hilo lilianza Agosti 5, 2016 saa tano usiku alipopokea simu kutoka kwa mmoja wa wafanyakazi wa hoteli ya SG Northern wakimweleza kuwa mtoto wa dada yake alikuwa hajachukuliwa hadi wakati huo, jambo ambalo si kawaida kwa kuwa dada yake humchukua mtoto saa 11 jioni.
Alidai mtoa taarifa huyo alimweleza kuwa walijaribu kumpigia lakini simu haikupokelewa, jambo ambalo hata yeye alilithibitisha na ilimpa hofu na kuamua kutoa taarifa kwa ndugu wengine.
Mrita alidai juhudi za kumtafuta kwenye baadhi ya vituo vya polisi vya hapo Arusha hazikuzaa matunda kwani walikosa ushirikiano lakini baadaye alipata taarifa kuwa nyumbani kwa dada yake kuna watu wameingia ambao wanazuia mawasiliano baina ya walio ndani na walio nje.
Alidai walipata hisia ni majambazi lakini bado walibaki hapo nje ambapo alishuhudia gari aina ya Land Cruiser ikitoka na baadaye kurudi kisha kuondoka tena.
"Tulikubaliana tusubiri hadi asubuhi kuanza kumtafuta tena kwenye vituo vya polisi lakini bado hatukufanikiwa kumpata hadi askari mmoja ambaye ninafahamiana naye aliponiambia 'nikwambie ukweli, ndugu yenu hayupo hapa Arusha wameshamsafirisha kwenda Dar’," alidai.
Alidai walisafiri kwenda Dar es Salaam, juhudi za kumtafuta kwenye vituo kadhaa hazikuzaa matunda na waliamua kwenda kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (wakati huo Diwani Athumani) ambaye ni ndugu wa bilionea Msuya na kumweleza kwamba dada yao alikuwa amepotea lakini naye hakuwapa jibu la kuridhisha.
"Nilipomweleza hali halisi aliniuliza kwani unahisi amekufa lakini hakunipa jibu la kunisaidia kujua ndugu yangu alipo hivyo niliamua kuondoka na kutafuta wakili na kazi ya kwanza tulimpa ilikuwa ni kutumia connection zake atusaidie kujua kama ndugu yetu yuko hai, kama yuko hai atusaidie kuonana naye," alidai.
Alidai kabla hawajapata majibu kutoka kwa wakili alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni RCO wa Arusha akimtaka akabidhi magari yote ya dada yake ambayo yalikuwa ni Range Rover mbili na Ford Ranger.
Mrita alidai kuwa baada ya muda alipokea simu kutoka kwa DCI ambaye alimtaka atekeleze alichoambiwa na RCO na asipofanya hivyo kwa hiari atatumia nguvu jambo ambalo walilitekeleza.
Aliendelea kudai kuwa baada ya tukio hilo waliendelea kumtafuta Miriam bila mafanikio hadi Agosti 15, 2016 alipopokea simu kutoka kwa wakili akimweleza wafike Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam wakutane na ndugu yao.
Miriam anashtakiwa kwa kumuua kwa kusudi Aneth Msuya, dada wa marehemu Msuya Mei 25, 2016 katika eneo la Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam.