Dk. Mwele Malecela, Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika vya Shirika la Afya Duniani (WHO)
KAKA yake aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), anayeshughulikia magonjwa yasiyopewa kipaumbele (NTDs), Dk. Mwele Malecela (58), Kasiandru Malecela amesema dada yake alipotolewa katika nafasi ya ukurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR) alichanganyikiwa kidogo lakini Dk. Mwele akawa anamfariji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Dk. Mwele aliyekuwa mtoto wa Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela, alikuwa Mkurugenzi (NIMR), ambapo uteuzi wake ulitenguliwa Desemba 2016 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.
Akitoa salama za shukrani kwa niaba ya familia leo tarehe 19 Februari, 2022, Kaka huyo amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amefanyia maajabu dada yake kiasi cha Watanzania kuguswa na msiba huo na kuomboleza kwa namna mbalimbali.
“Wanasema kitu ulichonacho huwezi kujua thamani yake mpaka kiondoke mikononi mwako.
“Baada ya msiba kutokea, nimekuwa nikisoma hizo rambirambi na watu wanavyoandika nikawa najiuliza hivi ni dada yangu huyuhuyu ninaye msikia hapa! Kwa kweli tunajivuni huyu dada yetu,” amesema na kuongeza;
“Tunashukuru wafanyakazi wenziwe kutoka WHO… kulipotokea kigugumizi kidogo huko NIMR mimi mmojawapo ambao nilichanganikiwa kidogo, lakini badala ya mimi kumfariji yeye, yeye akawa alinifariji mimi.
“Haikupita muda akapata kazi huko WHO, akaniambia kaka unaona mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu ana mpango na binadamu wake,” amesema.
Amesema kwa mipango ya Mwenyezi Mungu, dada yake alifanya kazi huko Congo Brazzaville na baadae akahamia Geneva Uswiss na kuwa bahati kwani alikuwa jirani naye.
Amesema matatizo yalipoanza kumpata Dk. Mwele ilikuwa ni rahisi kukimbia kwenda kumuona na kumfariji.
“Lakini unafika yeye ndio anakuambia kaka hii itapita tu wala usiwe na wasiwasi,” amesema.
Akinukuu maneno ya Askofu aliyeendesha ya kuaga mwili huo hapa jijini Dar es Salaam, Kaka huyo amesema binadamu tunapaswa kuondoka kwa mazuri kama ilivyo kwa dada yake.
Aidha, amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros kwani wakati wa ugonjwa hadi umauti unamfika Dk. Mwele alikuwa naye bega kwa bega, wafanyakazi wa ubalozi waliopo Geneva, kwa niaba ya familia jumuiya ya Watanzania waliopo Switzerland.
Pamoja na mambo mengine amesema wamepata pengo kubwa.
Aidha, kaka huyo amesema Dk. Mwele alianza kuugua alipotoka kwenye harusi ya binti yao Uholanzi.
“Mwele alikuwa dada na mtu spesho zaidi ya kwangu. Tumekuwa tukichangiana mambo mbalimbali ya familia, siku zake za kipindi cha kucheka ilikuwa harusi ya binti yetu.
“Asante sana watanzania wote kwa kumpa sifa anazostahili dada yangu. Mwenyezi Mungu umrehemu dada yangu,” amesema.
Jumatatu ya tarehe 21 Februari 2022, itafanyika misa takatifu kwenye Kanisa la Anglican Dodoma Cathedral, kisha mwili utapelekwa Kata ya Mvumi, kwenda kutolewa heshima za mwisho kwa watu wa wilaya ya Chamwino.
Hadi umauti unamfika, alikuwa anasimamia miradi ya kupunguza magonjwa ya kitropiki yasiyopewa kipaumbele ya WHO, jukumu alilolishika kuanzia Oktoba 2018. Alijiunga na shirika hilo la afya duniani mwishoni mwa 2016.