Kesi ya Mbowe: Inspekta Swila akana kuwa mpelelezi wa kimkakati



MKAGUZI wa Jeshi la Polisi Tanzania, Tumaini Swila, amedai uhamisho wake wa muda kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Temeke kwenda Makao Makuu Ndogo ya Upelelezi Dar es Salaam haukuwa wa kimkakati kwa ajili ya maandalizi ya kesi ya ugaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa makomando wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Inspekta Swila ametoa kauli hiyo leo Jumanne, tarehe 8 Februari 2022, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, iliyopo Mawasiliano jijini Dar ea Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Ni baada ya Wakili wa utetezi, Fredrick Kihwelo, kumuuliza kama atakuwa sahihi akisema uhamisho wake ni wa kimkakati, kwa ajili ya maandalizi ya kesi hiyo namba 16/2021, yenye mashtaka sita ya ugaidi.


 



Kihwelo alimhoji swali hilo Inspekta Swila, anayedaiwa kufungua jalada la kesi hiyo tarehe 18 Julai 2020, baada ya kudai alipata uhamisho wa muda ambapo alikuwa Makao Makuu Ndogo ya Upelelezi Dar es Salaam, kuanzia Januari 2020 hadi Agosti 2021, aliporejea katika kituo chake cha kazi.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, Ijumaa iliyopita, Inspekta Swila alidai alikuwa mpelezi msaidizi wa kesi hiyo, akimsaidia aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Ramadhan Kingai.

Mahojiano kati ya Wakili Kihwelo na Inspekta Swila ilikuwa kama ifuatavyo;

Kihwelo: Kwenye maelezo yako ulisema Januari 2020 ulipata uhamisho wa muda kwenda makao makuu ndogo ya polisi dar ni shaihi?


Shahidi: Sahidi

Kihwelo: Ni sahihi kuwa Agosti 2021 ulirudi kwenye kituo chako cha kazi?

Shahidi: Sahihi.

Kihwelo: Huu uhamisho wako ulikuwa wa muda gani shahidi?

Shahidi: Muda wa mwaka mmoja na miezi isiyozidi nane.

Kihwelo: Unaweza ukamwmabia Jaji ikiwa kuna nyaraka yoyote umeileta inayothibitisha ulipata uhamisho wa muda mfupi?


 
Shahidi: Sijaleta

Kihwelo: Unaweza ukamwambia jaji unavyojua suala la uhamishoni ni mchakato au ni tukio?

Shahidi: Una maanisha nini? Sijakuelewa.

Kihwelo: Yaani unapohamishwa unapitia taratibu mbalimbali au unaamka ukiwa Temeke halafu unajikuta Makao Makuu ndogo ya Polisi?

Shahidi: Ni utaratibu wa kazi.

Kihwelo: Twende kwenye utaratibu, wakati wa mahojiano yako uliiambia mahakama hii kwamba wakati wa uhamisho ulipitia taratibu mbalimbali?


Shahidi: Rudia swali lako.

Kihwelo: Wakati wa mahojiano yako uliijulisha mahakama hii unapohama kutoka Temeke kwenda Makao Makuu ndogo Dar es Salaam, ulipitia taratibu ulizozungumza?

Shahidi: Ndiyo nimeeleza.

Kihwelo: Nitakuwa sahihi nikisema dalili zote zinaonyesha kwamba timing ya uhamisho wako ilikuwa ya kimkakati na ilihususu maandalizi ya shauri hili?

Shahidi: Si kweli.

Kihwelo: Ulisema taarifa za matukio ya matendo ya kihalifu zilipokelewa na DCI Boaz?

Shahidi: Sahihi.

Kihwelo: Ilikuwa maandamano?

Shahidi: Ndiyo na matukio mengine.

Kihwelo: Ilikuwa na kudhuru viongozi?

Shahidi: Ndiyo na matukio mengine.

Kihwelo: Katika orodha hiyo niliyoitaja kuna ugaidi hapo?

Shahidi: Fafanua swali lako.

Kihwelo: Umetaja vitendo vilivyokuwa vifanywe katika orodha hiyo uliyoikubali, kuna ugaidi?


 
Shahidi: Makosa yaliyokuwa yanaambatana na kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi.

Kihwelo: Kuna ugaidi shahidi?

Shahidi: Ndiyo upo.

Kihwelo: Umeeleza pia viongozi ambao walipaswa kudhuriwa, unaweza mkumkubusha jaji viongozi hao ni wepi?

Shahidi: Kiongozi moja wapo ni Lengai Ole Sabaya.

Kihwelo: Wa pili?

Shahidi: Kwa taarifa zilizokuwepo awali alikuwepo Sabaya.

Kihwelo: Kwa hiyo huyo ndiyo viongozi?

Shahidi: Mmoja wa viongozi waliopangwa kudhuriwa.

Kihwelo: Taja wengine?

Shahidi: Wengine sifahamu.

Kihwelo: Kwa hiyo ulikuwa unaandika ambao hauwafahamu?

Shahidi: Nawafahamu.

Kihwelo: Hebu tuambie mtuhumiwa wa kwanza, pili na wa tatu, wewe unavyodhani wameshiriki vipi katika kuandaa maandamano au kuhamasisha maandamano?

Shahidi: Wanafahama walivyokuwa wanafanya.

Kihwelo: Wewe hufahamu namna gani wangeweza andaa maandamano?

Shahidi: Ni vitendo walivyovipanga kwenda kufanya wao

Kihwelo: Unafahamu hufahamu?

Shahidi: Ninachofahamu wanataka kufanya maandamano nchi nzima

Kihwelo: Kuandamana ni kosa?

Shahidi: Si kosa kama watafuata sheria.

Kihwelo: Wewe ulijuaje kwamba wataandamana bila kufuata sheria?

Shahidi: Kutokana na matendo mengine ambayo yalipangwa kufanyika ambayo yangeleta taharuki nchini.

Kihwelo: Kwnai walikuwa wameshaanza kuandamana?

Shahidi: Ilikuwa bado.

Kihwelo: Ulijuaje kama hawataomba kibali cha maandamano?

Shahidi: Hilo siwezi kujibu.

Shahidi huyo ananendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo, mbelw ya Jaji Tiganga.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad