Kesi ya Mbowe: Mamia Wafurika, Wazuiwa Getini




MAMIA ya wanachama wa Chadema, wamefika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam, kusikiliza uamuzi mdogo wa kesi ya uhujumu uchumi, namba 16/2022, inayomkabili Mwemyekiti wao, Freeman Mbowe na walinzi wake watatu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar ea Salaam … (endelea).

Uamuzi huo utatolewa leo Ijumaa, tarehe 18 Februari 2022, mahakamani hapo kuanzia saa 8.00 mchana na Jaji Joachim Tiganga anayeisikiliza kesi hiyo.

Ni uamuzi kama Mbowe na wenzake wana kesi ya kujibu au la, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao kwa kutumia mashahidi 13 kati ya 24 iliyopanga kuwatumia.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa makomando wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Lasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.



Wakati zaidi ya wanachama 480 wa Chadema, wakifanikiwa kuingia ndani ya mahakama hiyo, wengine wamezuiwa getini ikidaiwa kwamba eneo la mahakama limejaa.

Wakiwa viwanja vya mahakama, wamekuwa wakiimba na kuzunguka huku na huko wakisuburi nini hatima ya kiongozi wao aliyekaa rumande zaidi ya siku 200.

Afisa wa Chadema, Salagana Bwire Nyangero, anayeratibu zoezi la usajili wa wananchama na viongozi, wanaofika mahakamani hapo kusikiliza kesi hiyo, amesema wanachama hao wametoka katika majimbo ya chama hicho, nchi nzima.


“Watu 480 wameshafika kutoka mikoa mbalimbali ambao wameshafika nategemea ikifika saa 7.00 mchana nitakuwa na watu 100,000,” amesema Salagana.




Idadi ya wanachama na viongozi wa Chadema, waliofika mahakamani hapo ni mara tatu ya wanachama wanaokuja mahakamani hapo kila siku, wakati kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa.

Inakadiriwa, awali wanachama na viongozi waliokuwa wanakuja kusikiliza kesi hiyo, ni kati ya 70 hadi 200.

Katika kesi hiyo, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, likiwemo la kushiriki vikao vya kupanga ugaidi, kupanga njama za kudhuru viongozi wa Serikali akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimankaro, Lengai Ole Sabaya. Kupanga maandamano yasiyo na kikomo nchi nzima.


Shtaka lingine linalowakabili pamoja ni la kutaka kuchoma vituo vya mafuta na mikusanyiko yenye maeneo ya watu.

Pia, Mbowe anakabiliwa na shtaka la kutoa fedha Sh. 699,000 kwa ajili ya kufadhili vitendo hivyo, wakati Kasekwa akikabiliwa na shtaka la kukutwa na silaha aina ya bastola, kinyume cha sheria na dawa za kulevya.

Huku Hassan akikabiliwa na shtaka la kukutwa na sare pamoja na vifaa vya JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai na Agosti 2020, kwenye mikoa ya Morogoro, Kilimanjaro na Dar es Salaam.


Jamhuri imeleta vielelezo vya ushahidi 39 na mashahidi 13 kati ya 24 iliyopanga kuwaita.

Hadi Jamhuri inafunga ushahidi wake, zimesikilizwa kesi ndogo mbili ndani ya kwai kubwa, ambazo ni zile za kupinga maelezo ya onyo ya Kasekwa na Ling’wenya, wakidai hayakuchukuliwa kwa mujibu wa sheria, lakini mahakama hiyo iliyapokea ikieleza yalichukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad