Kesi ya Mbowe Niliyafanyia Kazi Maneno ya Kusikia Kufungua Kesi Ugaidi



SHAHIDI wa 13 upande wa Jamhuri, Inspekta Tumaini Swila, ameligusa shtaka la kula njama kuchoma masoko na kulipua mikusanyiko ya watu baada ya kukiri kwamba katika maelezo yake, maelezo ya ACP Ramadhani Kingai, SP Jumanne na Luteni Urio, hakuna sehemu waliyosema washtakiwa watafanya hayo.

Inspekta Swila amekiri kwamba alifanyia kazi maneno ya kusikia kwa Kamishna wa Polisi Robert Boaz aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), akafungua jalada la kesi ya ugaidi bila ya kuwa na maelezo ya mlalamikaji huyo (Boaz).

Shahidi alidai hayo jana Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Joackim Tiganga wakati akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibata katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Alidai alichukua sampuli nne za mshtakiwa Halfani Bwire kupeleka kwenye uchunguzi kwa maelekezo ya Afande Kingai.
Shahidi huyo alidai alisomea mchakato wa uchukuaji wa sampuli katika Chuo cha Taaluma ya Polisi lakini yeye si mchunguzi.

Alidai kuwa nyumbani kwa Bwire, walichukua sampuli ya notebook lakini Kingai hafahamu na aliikabidhi kwa Sajenti Johnson kwa utaratibu wa kipolisi.


 
Wakili Kibatala alihoji akitaka kujua michoro ya ramani katika notebook ya Bwire aliichora kabla ya kukutana na Luteni Urio na Mbowe au la, shahidi akidai kwake hilo halikuwa muhimu kwa kuwa jambo la msingi kwake lilikuwa kujua mwandiko ni wa nani.

Alidai kidaftari hicho hakitakuwa muhimu kwenye kesi hiyo ya ugaidi kama mshtakiwa Bwire alichora michoro hiyo Mei 5, mwaka 2020.

Akiendelea kuhojiwa, shahidi huyo alidai alifungua jalada la kesi Julai 18, mwaka 2020, kabla hajamhoji Kamishna Boaz ambaye alihojiwa Oktoba 13, 2020 ikiwa ni baada ya miezi mitatu baada ya jalada kufunguliwa.


Inspekta Swila alidai hakuwapo wakati Luteni Urio anatoa taarifa za ugaidi kwa Kamishna Boaz na alikiri kuwa alifanyia kazi maneno ya kusikia kutoka kwa Boaz.

Alidai alifungua jalada akiwa na taarifa ya kesi ya ugaidi ambayo alipokea kutoka kwa Kamishna Boaz.

Alipohojiwa sababu za kufungua kesi kabla ya kuchukua maelezo ya mlalamikaji, shahidi huyo alidai ikiwa kesi imefunguliwa na raia, lazima maelezo yachukuliwe kwa haraka lakini kama ni polisi, maelezo sio lazima yachukuliwe kwa haraka.

Wakili Kibatala akataka shahidi aonyeshe ni kifungu gani katika Mwongozo wa Jeshi la Polisi (PGO) kinaonyesha tofauti hiyo.


 
Shahidi alipewa PGO asome eneo hilo, lakini alidai hakumbuki lakini alisoma eneo lingine ambalo mwongozo unamtaka polisi aliyepokea taarifa kuandika maelezo ya mtoa taarifa yoyote.

Inspekta Swila alidai hoja ya Kibatala kwamba walimkamata Luteni Urio na wakampiga baada ya kutajwa na mshtakiwa wa pili, Adamu Kasekwa maarufu Adamoo kisha wakampa dili la kuwa shahidi, si ya kweli.

Alidai kuwa wakati anafungua jalada la uchunguzi, Afande Kingai hakumwambia kwamba kuna tuhuma za ugaidi na si yeye aliyeamua kufungua jalada la kesi ya ugaidi.

Wakili Kibataka alimpa maelezo ya wapelelezi wenzake aonyeshe sehemu waliyosema washtakiwa watachoma masoko na kulipua mikusanyiko ya watu.


Akijibu hoja hiyo, shahidi huyo alidai katika maelezo ya Afande Kingai na Luteni Urio hakuna sehemu ambayo wamesema washtakiwa watachoma masoko.

Alidai kuwa katika maelezo ya Afande Jumanne, hakuna sehemu inayosema watachoma masoko na katika maelezo yake, hakuna sehemu aliyoandika kwamba washtakiwa watalipua mikusanyiko ya watu.

Inspekta Swila alidai kuwa baada ya kufungua jalada la kesi, DCI Boaz alimtaka kuwa mpelelezi katika shauri hilo la ugaidi na alichukua maelezo mbalimbali ikiwamo maelezo ya Luteni Urio.

Alidai hakuna mahali kulikoandikwa alikuwa msaidizi wa Afande Kingai ama Kingai kushirikiana naye katika kufanya upelelezi.

Akizungumzia bastola inayodaiwa alikamatwa nayo mshtakiwa Adamu Kasekwa kule Moshi aina ya Luger yenye namba A5340, shahidi huyo alidai hakuwahi kuitambua kwa maneno CZ100 CALLBRE kutoka mdomoni kwake.


 
Awali akihojiwa na Wakili Fredrick Kihwelo, shahidi alidai kiongozi aliyetaka kudhuriwa ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, na hawajui viongozi wengine waliotaka kudhuriwa.

Shahidi huyo alidai kufanya maandamano sio kosa kama utaratibu ukifuatwa lakini kwa upande wa kesi hiyo washtakiwa ndio wanajua kama walipanga kufanya maandamano.

Washtakiwa katika shauri hilo ni Mbowe, Bwire, Kasekwa na Mohammed Ling'wenya ambao wanadaiwa kula njama kufanya vitendo vya kigaidi ikiwamo kulipua vituo vya mafuta, mikusanyiko ya watu, kuchoma masoko na kuwadhuru viongozi wa serikali kati ya Mei Mosi na Agosti 5, 2020.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad