Kibatala alivyotumia saa 11 kumhoji Luteni Urio



Dar es Salaam. Kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi Peter Kibatala  ametumia jumla ya saa 11 na dakika mbili kumhoji maswali shahidi wa 12 upande wa mashtaka, Luteni Denis Urio katika kesi ya ugaidi inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Kibatala alitumia muda huo kumhoji shahidi huyo kwa siku tatu tofauti kuanzia Ijumaa iliyopita mchana, baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake.

Wakati Kitabala akitumia muda huo kumhoji shahidi yeye pekee mawakili wengine watatu wote kwa pamoja walitumia jumla ya saa 4 na dakika 14.

Mawakili hao ni Nashon Nkungu kwa niaba ya mshtakiwa wa kwanza, aliyetumia saa moja na dakika 35, John Mallya kwa niaba ya mshtakiwa wa tatu, saa moja na dakika 38 na Dickson Matata kwa niaba ya mshtakiwa wa tatu, saa moja na dakika moja.


 
Hivyo mawakili wa utetezi kwa ujumla wao walitumia jumla ya saa 15 na dakika 16 kumhoji shahidi huyo maswali kwa nyakati tofauti, huku Kibatala akiweka rekodi ya kutumia muda mwingi zaidi kumhoji maswali shahidi kuliko shahidi mwingine yeyote katika kesi hiyo.

Muda huo uliotumiwa na mawakili kumhoji maswali shahidi huyo (cross examination) unamfanya kukaa kizimbani kutoa ushahidi kwa jumla ya saa 22 na dakika 14.

Muda huo unajumuisha na muda alioutumia kutoa ushahidi wa msingi au ushahidi mkuu, wakati akihojiwa na mwendesha mashtaka, yaani jumla ya saa 6 na dakika 38 na muda alioongozwa na mwendesha mashtaka kufafanua mambo yaliyoibuliwa na mawakili wa utetezi (re examination),dakika 20.


Kwa nini shahidi huyo ametumia muda wote huo

Mawakili hao wa utetezi akiwamo Kibatala na waendesha mashtaa wametumai muda mrefu kwa shahidi huyo kutokana na umuhimu wa ushahidi wake.

Luten Urio ambaye ni Afisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kutoka kikosi maalumu (makomando) kilichoko Ngerengere, mkoani Morogoro, ndiye shahidi muhimu namba moja katika kesi hiyo.

Yeye ndiye msingi wa kuwepo kwa kesi hiyo.


 
Hii ni kwa sababu yeye ndiye aliyeibua tuhuma za njama za uhalifu huo zinazowakabili washtakiwa, kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boazi, wakati huo (kwa sasa mstaafu)

Upande wa mashtaka ulitumia muda mwingi katika kujenga kesi yake ili kuhakikisha kuwa kila jambo la msingi wameliweka bayana ili kuthibitisha mashtaka bila kuacha mashaka yoyote.

Mawakili wa utetezi pia kwa upande wao, walitumia muda mwingi kuhakikisha kwamba hawaachi jiwe juu ya jiwe bila kupinduliwa kwa kumbana maswali yenye kuonesha udhahifu kwa kila hoja ya ushahidi wa shahidi huyo.

Muhtasari wa ushahidi wake     

Katika ushahidi wake mkuu, akiongozwa na mwendesha mashtaka,


Chavula, shahidi huyo alieleza kuwa alifahamiana na Mbowe mwaka 2008, baada ya Mbowe kumpigia simu na kujitambulisha kwake kisha akamuuliza kuhusu wasifu wake, huu akimweleza kuwa wanatoka eneo moja, Moshi.

Luteni Urio alieleza kuwa tangu mwaka huo waliendelea kuwasiliana tu kwa simu na Mbowe ambaye alikuwa wakati mwingine akimtumia ujumbe wa kumtakia heri kuhusiana na matukio mbalimbali yakiwemo sikukuu.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Joachim Tiganga, Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021 ni Halfan Bwire Hassan (wa kwanza), Adamu Hassan Kasekwa (wa pili) na Mohamed Abdillahi Ling’wenya (wa tatu), ambao waliachishwa kazi Jeshi la Wananchi (JWTZ) kikosi cha makomandoo, kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashtaka sita, mawili ya kula njama kutenda vitendo vya kigaidi vinavyodaiwa kutishia amani na usalama wa wananchi kwa lengo la kusababisha hofu kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,(washtakiwa wote).


 
Vitendo hivyo ni kulipua vituo vya mafuta na maeneo ya mikusanyiko mikubwa ya watu Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Kilimanjaro, kumdhuru aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya,  maandamano yasiyokoma na kuzuia barabara kwa miti na magogo.

Mengine ni kushiriki vikao vya vitendo vya kigaidi (washtakiwa wote), kufadhili vitendo vya kigaidi (Mbowe),kukutwa na mali za kutekelezea vitendo vya ugaidi bastola(Kasemwa) na sare na vifaa vingine vya Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa Halfani.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti Mosi na Agosti 5, 2020 katika Hotel ya Aishi wilayani Hai mkoani Kilimanjaro na katika maeneo mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Arusha.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad