Serikali imesema vichwa vya treni ya umeme vilivyoagizwa bado havijawasili nchini.
Imesema vichwa hivyo vipo kiwandani vinatengenezwa, kilichoingia nchini ni cha wakandarasi kwa ajili ya kufanyia majaribio.
Kauli hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa baada ya kuibuka mjadala kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kichwa cha treni kilichoingia nchini.
Katika ukurasa wake wa twitter, Msigwa ameandika: “MSIPOTOSHE. Vichwa vya treni ya umeme vilivyoagizwa na Serikali bado havijawasili nchini, bado vipo kiwandani vinatengenezwa. Kichwa cha treni ya umeme kilichokuja ni cha wakandarasi kwa ajili ya majaribio ya reli ya kisasa ya SGR.”
Februari 21, mwaka huu, katika ukurasa wake wa Twitter, Msigwa aliandika: “Kichwa cha treni cha umeme chawasili nchini. Ni kitakachotumika katika reli mpya ya kisasa (SGR).”
Baada ya kupost uliibuka mjadala kutoka kwa watu mbalimbali wakimuhoji Msigwa kwamba kichwa hicho ni chakavu.