IMEELEZWA kuwa, kigogo mwenye ushawishi wa fedha na usajili ndani ya Yanga, amewaita Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kwa ajili ya kujadili hatima ya kumpa mkataba kiungo Mghana, Bernard Morrison.
Kiungo huyo hivi sasa yupo katika mgogoro na mabosi wake wa Simba ambapo wiki iliyopita walitangaza kumsimamisha kwa makosa ya utovu wa nidhamu.
Mghana huyo aliyewahi kucheza Yanga kwa muda wa miezi sita kabla ya kuhamia Simba msimu wa 2020/21, inaelezwa yupo katika mazungumzo ya mwisho na timu yake hiyo ya zamani baada ya mkataba wake na Simba
kutarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Mmoja wa mabosi wa Yanga mwenye ushawishi mkubwa katika usajili, ameliambia Spoti Xtra kuwa, viongozi wa Kamati ya Utendaji wamepanga kukutana kujadiliana hatima ya kumsajili huyo, huku kukiwa na kigogo
ambaye yupo tayari kutoa Sh 230Mil kufanikisha dili hilo.
Bosi huyo alisema lengo la kigogo huyo kukutana na viongozi wa kamati hiyo ni kuwashawishi baadhi yao
kukubali baada ya wengine kuonekana kukataa kiungo huyo kurejeshwa kikosini hapo kutokana na kuondoka vibaya.
Aliongeza kuwa, kikao hicho ndiyo kitaamua hatma ya Morrison, licha ya mazungumzo baina ya mchezaji na viongozi kufikia pazuri.
“Kama unavyofahamu Morrison aliondoka Yanga vibaya sambamba na kupelekwa kesi yake CAS
kupinga uamuzi wa TFF ambao ulimuidhinisha kiungo huyo kwenda Simba licha ya kuwa na mkataba na Yanga.
“Kuondoka huko vubaya ndiyo kumewakera baadhi ya viongozi na kuchukua uamuzi wa kuzuia kiungo huyo asirejee Yanga, licha ya kigogo huyo kugharamia usajili wake wote.
“Hivyo Kamati ya Utendaji itakutana na kigogo huyo kwa ajili ya kumjadili Morrison na uamuzi utakaofikiwa ndiyo utakuwa wa mwisho, lakini upo uwezekano mkubwa wa kiungo huyo kurejea Yanga,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema: “Hizo taarifa tunazisikia kwenye mitandao, lakini kama uongozi ni lazima kila usajili tuujadili kabla ya
kumsajili mchezaji.
“Uongozi bado haujakutana kuzungumzia usajili wa Morrison, hivyo tusubirie Kamati ya Utendaji itakapokutana ndiyo tutakuwa na majibu mazuri ya hayo, lakini ikumbukwe kuwa mchezaji huyo ana mkataba na Simba.”
STORI NA WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA