Kilichomkuta Chama Baada ya Kurudi Simba



CLATOUS Chama amerejea Simba lakini si kwa kiwango kile alichoondoka nacho kwenda RS Berkane, na anahitaji muda zaidi ili awe kwenye ubora wake huku Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola akiweka wazi sababu kuwa ni kiungo huyo kutopata muda mwingi wa kucheza kule Morocco.

Akizungumza na Mwanaspoti, Matola alisema kuwa nyota huyo hajawa fiti kwa kiwango kikubwa hivyo itamchukua muda kurejesha makali yake yaliyozoeleka.

“Hakuna asiyejua ubora wa Chama awapo uwanjani na isitoshe hakupata muda mwingi wa kucheza kule, lakini kadri anavyozidi kupata muda inazidi kumjengea hali ya kujiamini na kufanya vizuri zaidi,” alisema Matola na kuongeza;

“Uwepo wake kwenye kikosi chetu umetuongezea wigo mpana wa wachezaji wabunifu hususani eneo la kiungo ambalo husaidia kuunganisha safu ya ushambuliaji licha ya kutofanya vyema michezo ya hivi karibuni changamoto ambayo kwa sasa tunaifanyia kazi,” alisema Matola.


Awali alipojiunga na Simba, Septemba 15, 2019, Chama, raia wa Zambia alikuwa muhimili mkubwa ndani ya kikosi hicho kabla ya kuondoka msimu uliopita kisha kurejea kwenye dirisha dogo lililopita.

Kiungo mchezeshaji huyo alifanya makubwa akiisaidia Simba kutisha kwenye michuano ya ndani na ile ya kimataifa, wakibeba mataji ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) huku akiwa miongoni mwa nyota walioipigania timu hiyo kufika hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kurejea kwake ni faida kwa timu hiyo kutokana na mchango wake wa kufunga na kupika mabao na hilo alilionyesha msimu uliopita kabla ya kuondoka kwani katika mabao 78 ambayo Simba ilifunga alihusika kwenye mabao 23, akifunga mabao nane na kutoa asisti 15.

Msimu wa 2021/22 amerejea tena wakati wa dirisha dogo la usajili la Januari na kucheza michezo minne ya Ligi Kuu Bara ambapo alianza dhidi ya Mtibwa Sugar walipotoka suluhu, walipolala 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na ushindi wa 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya Kwanza Februari waliyoshinda pia 1-0, bao alilofunga yeye.

Chama pia ana dakika 540 za kuisaidia timu yake kupata matokeo chanya katika michezo ya Kombe la Shirikisho Afrika inayotarajiwa kupigwa mwezi huu wakianza na Asec Mimosas ya Ivory Coast itakayochezwa Februari 13 kwenye Uwanja wa Mkapa huku wakicheza mechi nyingine ya hatua ya 16 ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Ruvu Shooting.

Baada ya hapo Simba itaenda ugenini kucheza na Gendarmerie Nationale (Nigeria) Februari 20, RS Berkane ya Morocco Februari 27 kisha itarejea nyumbani kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Biashara United Machi 3 na kurudiana na RS Berkane Machi 13 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad