Ilianza kama masihara, chokochoko zikapamba moto na sasa, tayari mashambulizi ya kijeshi ya majeshi ya Urusi yameanza rasmi katika ardhi ya Ukraine hususan katika Mji Mkuu, Kyiv na katika majimbo mawili yanayotaka kujitenga.
Urusi imeamua kuweka pamba masikioni na kutosikiliza ushauri wa mataifa mengi wa kuisihi isianze oparesheni zake za kivita dhidi ya Ukraine ili kuzuia madhara yanayoweza kuletwa na vita! Rais Vladmir Putin ameamua kutunisha misuli na sasa tayari vita kamili imeanza.
Urusi imeeleza kwamba Februari 23, 2022 imeishambulia miundombinu ya kijeshi, vifaa vya ulinzi wa anga na viwanja vya ndege vya kijeshi vya Ukraine kwa kutumia silaha nzito hususan katika Jiji la Kiev ambapo ndipo yalipo makao makuu ya Ukraine.
Kwa upande wake, Ukraine nayo haijataka kuonyesha unyonge, bunge la nchi hiyo limepitisha azimio la nchi hiyo kuwa katika hali ya hatari kwa siku 30 kuanzia hapo jana, Februari 23, 2022 kutokana na mashambulizi yaliyofaanywa na Urusi kwenye ardhi yake.
Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine mara kadhaa amesikika akieleza kwamba kamwe nchi yake haiogopi vitisho vya Urusi na itakabiliana na mashambulizi yoyote itakayoyafanya.
Tayari jeshi la Ukraine limeanza kujiandaa kujibu mashambulizi ya Urusi, ambapo sheria maalum ya kijeshi, martial law imetangazwa nchi nzima, wanaume wote wenye umri wa miaka kumi na nane wametakiwa kujiunga haraka na jeshi ili kupata mafunzo ya haraka ya utayari na vikosi vyenye silaha nzito vya Ukraine, vimekaa tayari kusubiri amri ya kuanza mashambulizi.
Je, hii ni ishara ya kuanza kwa vita ya tatu ya dunia? Rais wa Marekani, Joe Biden amesikika akitangaza kwamba nchi yake itaisaidia Ukraine kupambana na Urusi na kumuonya Rais wa Urusi, Vladmir Putin kwamba atawajibishwa kwa hatua zake za kichokozi anazozichukua dhidi ya Ukraine.
Baraza la usalama la umoja wa mataifa, nalo limeitisha kikao cha dharura na kwa kauli moja, limekemea vikali hatua za kijeshi zilizochukuliwa na Urusi. Kwa upande wa majeshi ya kujihami ya NATO, nayo tayari yameonesha msimamo wa kuisaidia Ukraine kupambana na Urusi.
Mashambulizi ya Urusi, yamekuja wiki kadhaa baada ya usalama kati ya mataifa hayo jirani, kuanza kuwa tete kutokana na Urusi kupinga hatua ya Ukraine kutaka kujiunga na NATO.
Urusi ilituma zaidi ya wanajeshi laki moja kwenye mpaka wake na Ukraine lakini licha ya hatua hiyo, ilikanusha kuwa na mpango wowote wa kuivamia nchi hiyo ambayo nayo iliweka vikosi vyake tayari kujibu mapigo. Ni dhahiri sasa kwamba Urusi ilikuwa imejipanga kisawasawa kuivamia Ukraine na maneno ya Putin, yalikuwa ni kama kuihadaa dunia kwamba hana nia ya kuivamia Ukraine.
Uchokozi wa Urusi ulizidi kushika kasi baada ya Rais Putin, kutangaza kuyatambua rasmi majimbo mawili yanayotaka kujitenga na Ukraine, Donetsk na Luhansk yaliyopo mashariki mwa nchi hiyo.
Ni nini kitakachoendelea? Macho na masikio ya dunia nzima kwa sasa ni nchini Ukraine! Muda utazungumza.
Imeandaliwa na Aziz Hashim kwa msaada wa mitandao.