Wanajeshi wa Rwanda wanaoshika doria Msumbiji kwenye picha ya awali
Shirika la habari la AFP linaripoti kwamba kiongozi wa kundi lenye msimamo mkali raia wa Tanzania anayehusika kuongoza mashambulizi ameuwawa nchini Msumbiji kwa mujibu wa tangazo la polisi la Jumatatu.
Tuahil Muhidim aliongoza shambulizi la mwaka 2020 la kusababisha kushikilia mji wa Macimboa da Praia, wa bandari ya kaskazini iliyokuwa ikitumiwa kupokea shehena ya mradi wa gesi wa mabilioni ya dola katika eneo hilo.
Kamanda wa polisi wa eneo hilo Bernadino Rafael amesema kupitia redio ya taifa kwamba vikosi vya Msumbiji na Rwanda vimemuua Muhidin, Jumapili asubuhi. Kiongozi huyo aliyeuwawa anashutumiwa pia kuhusika na kuteka watawa wawili wa Kibrazili kwa wiki zaidi ya tatu mwaka 2020.
Katika oparesheni hiyo, vikosi vya usalama vimemuua mwanamgambo mwingine na kukamata bunduki mbili. Wanamgambo walizuka kaskazini mwa Msumbiji katika mpaka na Tanzania na kufanya mashambulizi.