Dar es Salaam. Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza wamegundua virusi vipya vya Ukimwi wanavyoita ‘VB variant’.
Wanasema virusi hivyo ni hatari zaidi ikilinganishwa na vile vilivyokuwepo katika sehemu tofauti duniani tangu miaka ya themanini na vimekuwapo nchini Uholanzi kwa muda mrefu.
Taarifa zaidi zinasema watu wanaoishi na aina hiyo mpya ya virusi, miili yao hudhoofika mara mbili ya kiwango cha kupungua kwa kinga mwili (CD4).
Pia, wana viwango vya juu vya virusi vya Ukimwi (kiasi cha virusi kwenye damu) na wanakuwa hatarini kusambaa haraka kwa VVU mara mbili hadi tatu baada ya kugundulika ikilinganishwa na kirusi cha zamani.
Utafiti huo ulioongozwa na Chuo Kikuu cha Oxfords katika taasisi yake ya takwimu, ulikuwa wa kwanza kugundua lahaja ndogo ya B ya virusi.
Pia imebaini lahaja hiyo imekuwa ikisambazwa nchini Uholanzi kwa miaka mingi na inakuwa ikipokea matibabu ya VVU.
Hata hivyo, Mganga Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Aifelo Sichwale akizungumza na Mwananchi kuhusiana na virusi hivyo juzi jioni, alisema bado hawana taarifa hizo, bali nao wameziona kwenye mitandao ya kijamii.
Alisema bado Shirika la Afya Duniani (WHO) halijatoa tamko kuhusu kuwapo kwa virus hivyo vipya na kwamba ndilo lenye jukumu la kutangaza ugonjwa mpya.
Hata hivyo, alisema wizara inaendelea kufuatilia uwapo wa magonjwa mbalimbali yakiwamo ya mlipuko yanayoripotiwa kwenye mataifa mengine, lakini pia hata magonjwa mengineyo. “Hivyo taarifa zitakapopatikana, mamlaka husika itatoa taarifa kwa umma. Tunaomba wananchi wasiwe na hofu badala yake waendelee kuchukua tahadhari na kutekeleza afua ya kujikinga na VVU/Ukimwi,” alisema Dk Sichwale.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Unaids, Eamonn Murphy alisema watu 10 milioni wanaoishi na VVU duniani kote, baadhi yao hawapati matibabu, hali inayochochea kuendelea kuenea kwa virusi hivyo na hiyo inatishia uwezekano wa kuwapo kwa aina nyingine zaidi ya virusi.
“Tunauhitaji wa dharura wa kupeleka ubunifu wa hali ya juu wa matibabu kwa njia zinazofikia jamii zenye uhitaji zaidi. Iwe ni matibabu ya VVU au chanjo ya Uviko -19, ukosefu wa usawa katika ufikiaji unaendeleza magonjwa ya milipuko kwa njia zinazotudhuru sisi sote,” alisema Murphy.
Kwenye ripoti iliyochapishwa Alhamisi wiki iliyopita kwenye jarida la Science, ilibainika kuwa watu walioambukizwa virusi hivyo vipya vya‘VB variant’, wana idadi ya virusi vya HIV mara tatu na nusu hadi tano na nusu ikilinganishwa na wale walioambukizwa vile vya kawaida.
Tafiti pia zimeonyesha virusi hivyo vipya vinapunguza uwezo wa mwili kujilinda dhidi ya maradhi mengine ikilinganishwa na wale walioambukizwa virusi vya kawaida.
Hata hivyo, utafiti ulionyesha baada ya watu walioambukizwa virusi hivyo na kuanza matibabu, wana nafasi sawa ya kupona na kuimarisha mfumo wa miili yao kukabiliana na magonjwa kama wale walioambukizwa virusi vya kawaida. “Watu wanapaswa kuwa na hofu kutokana na kugundulika kwa virusi hivi vipya,” alisema Chris Wymant ambaye ndiye aliyeongoza wataalamu hao kwenye utafiti.
Wataalamu hao walisema kuna uwezekano virusi hivyo vilianza kusambaa mwishoni mwa miaka ya themanini na mapema tisini, lakini vikaanza kupungua tangu mwaka 2010.
Walisema wanaamini uwepo wa mbinu za kisasa za matibabu utasaidia pakubwa kukabili maambukizi yake.
Walieleza wanaamini kuwepo kwa virusi hivyo Uholanzi haujachangia maenezi yake katika sehemu nyingine duniani, japo kuna haja kwa mataifa mengine kuboresha mikakati ya kuvikabili. “Matokeo ya utafiti huo yanasisitiza kuhusu haja ya WHO kuwahamasisha watu kuhusu haja ya kupimwa mara kwa mara ikiwa wameambukizwa virusi hivyo.
“Hili litawasaidia kuanza matibabu ya mapema ikiwa watabainika kuambukizwa,” alisema Christopher Fraser ambaye pia alishiriki kwenye utafiti huo.