Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Kasheku Musukuma amemshukia Rais wa Shirikisho la soka nchini TFF Wallace Karia kwa kumtuhumu kuwa adui namba moja wa kuua soka la Tanzania, kufuatia kujiondoa kwa Mdhamini Mwenza wa Ligi Kuu Tanzania Bara Kampuni ya GSM.
Musukuma ametoa tuhuma hizo kwa ujumbe wa sauti aliousambaza katika mitandao ya kijamii, huku akionesha kusikitishwa na hatua zilizochukuliwa na Kampuni ya GSM juzi Jumatatu (Februari 07).
Musukuma amesema Karia ameshindwa kuongoza soka la Tanzania na anapaswa kujiuzulu, kutokana na baadhi ya mambo kufanywa hadharani kwa makusudi na yeye kama kiongozi anayakalia kimya.
Mbali na tuhuma kwa kiongozi huyo, Musukuma amelaani vitendo vya baadhi ya waamuzi wanaochezesha michezo ya Ligi Kuu kwa kushindwa kusimamia sheria 17 za mchezo wa soka na kujikuta wakizionea baadhi ya timu ambazo zinajiandaa kwa gharama kubwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kampuni ya GSM ilitangaza kuondoa udhamini wake kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es salaam kwa kigezo cha baadhi ya vipengele vya mkataba uliosainiwa Mwezi Novemba mwaka jana dhidi ya TFF havijafuatwa.