MATHIAS Lule, Kocha Mkuu wa Mbeya City, amesema kuwa waliingia uwanjani kuwavuruga Yanga baada ya kujua kwamba wamewasoma kwenye mechi zao ambazo wamecheza.
Juzi, Mbeya City iliweza kusepa na pointi moja mbele ya Yanga ambao ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 36 baada ya kucheza mechi 14 msimu wa 2021/22 na hawajapoteza mchezo.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Lule alisema kuwa alikuwa anatambua ubora wa Yanga ulipo na namna bora ya kuwavuruga jambo ambalo limewafanya wapate pointi moja ambayo kwao ni muhimu.
“Yanga ubora wake ni eneo la kati na ukiwaacha wacheze wao wanacheza kwa kujiamini, hivyo tulichokifanya ni kuwavuruga kwenye kila kitu, hiyo ilikuwa ni mpango kazi wetu, ndiyo maana unaona kwamba hata mipira iliyokufa tulikuwa tunaitumia bila kuleta hatari kwao.
“Kikubwa ilikuwa ni kuanza na mfumo wa kujilinda kisha kushambulia kwa kushtukiza na kuwabana kwenye eneo la viungo ambalo limekuwa likitumika kupata ushindi. Wao walitusoma kwenye mechi zetu tukabadili mbinu wakakutana na kitu cha tofauti,” alisema Lule.
Mbeya City imesepa na pointi nne mbele ya vigogo Simba na Yanga msimu wa 2021/22 baada ya kuwatungua Simba bao 1-0 Uwanja wa Sokoine kisha ikawa ni sare ya bila kufungana na Yanga, Uwanja wa Mkapa, juzi.