Korea Kaskazini imerusha kombora linalodhaniwa kuwa la masafa marefu kuelekea baharini, katika muendelezo wa majaribio yake ya silaha baada ya kumalizika kwa Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi nchini China.
Majaribio hayo ni ya nane mwaka huu huku baadhi ya wataalam wakisema kwamba Korea Kaskazini inajaribu kukamilisha teknolojia yake ya silaha na kuishinikiza Marekani kutoa makubaliano kama vile kuiondolea vikwazo.
Wakuu wa vikosi vyote vya majeshi nchini Korea Kusini, wamethibitisha juu ya Korea Kaskazini kurusha makombora lakini hawakutoa maelezo zaidi. Ofisi ya rais imesema inapanga kufanya mkutano wa dharura wa baraza la usalama la taifa kujadili uzinduzi huo.