KIKOSI cha Simba kipo Niger kikiwa na matumaini kibao dhidi ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Gendarmarin, huku kocha mkuu Pablo Franco akikunya mkwanja wa maana.
Kocha huyo pi atavuna mamilioni zaidi kulingana na mkataba wake iwapo ataivusha timu hiyo kuingia robo fainali ya michuano hiyo ya Afrika, kwani atapewa atapewa bonasi ya Dola za Kimarekani 10,000 (zaidi ya Sh20 milioni).
Ikiivusha Simba hatua ya nusu fainali atapata bonasi ya Dola 15,000 (zaidi ya Sh30milioni) na kama watafika fainali atavuta bonasi ndefu zaidi ya Dola 20000 ambayo ni zaidi ya Sh40 milioni
Habari kutoka Simba, zinasema kuwa Pablo amevuna mkwanja wa maana kwa ushindi wa mechi zote za nyumbani, kwani kila timu ikishinda anakunja si chini ya 400,000, huku kimataifa ndio balaa zaidi.
Bonasi hizo za kila mwisho wa hatua Pablo atakazovuta tofauti kabisa na zile ambazo atachukua kila baada ya mechi kwenye hatua ya makundi ambazo watashinda na mgao wake utakuwa sawa na mchezaji aliyecheza.
Kwani kwa mujibu ya taarifa hizo za ndani zinasema kuwa, mkataba wa Pablo unaonyesha anatakiwa kupewa bonasi katika mechi zote za ligi watakazoshinda sawa na mchezaji aliyecheza katika mechi hiyo.
Simba kila mechi ya ligi wakishinda wachezaji wanapata bonasi ya Sh20 milioni na mchezaji aliyecheza hata dakika moja mgawo wake unakuwa Sh400,000 ambayo pia Pablo anatakiwa kupata kiasi hicho.
Pablo tangu ametua nchini amekiongoza kikosi cha Simba kwenye mechi kumi za Ligi Kuu Bara kati ya hizo ameshinda sita ambazo ukizidisha na Sh400,000 maana yake atakuwa amevuna Sh2.4 kama bonasi yake.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez aliliambia Mwanaspoti kuwa, wamefanya hilo kutokana na kuwarahisishia kazi wachezaji na benchi la ufundi ili kuwa na kiu ya kufanya vizuri katika kila mechi.
“Tuna imani jambo hili la bonasi linao ngeza hali ya ufanyaji kazi kwa kila mmoja na kushinda kila mechi ili kutimiza malengo ya timu yetu,” alisema Barbara.