Leo ni zamu ya Misri, Cameroon kuraruana
NA MASHIRIKA
MAJABALI Misri na wenyeji Cameroon watakutana katika nusu-fainali ya kukata na shoka ya Kombe la Afrika (AFCON), uwanja wa Olembe mjini Younde, Cameroon, leo usiku.
Wakati Misri wakijivunia staa Mohamed Salah, Cameroon watamtegemea Vincent Aboubakar kuongoza mashambulizi.
Timu hizo zimekutana mara nyingi zaidi katika awamu ya muondoano ya Afcon; huku Cameroon ikiibuka na ushindi wa 2-1 mara ya mwisho zilipomenyakana kwenye fainali ya 2017 nchini Gabon.
Zote zimetinga hatua hii kutokana na msaada mkubwa wa wawili hao ambao huchezea klabu za Liverpool nchini Uingereza na Al-Nassr ya Saudi Arabia mtawaliwa.
Huku Aboubakar akianza kwa kasi ufungaji wa mabao katika dimba hili, Salah ameona nyavu mara mbili pekee baada ya vikosi kumwekea ukuta mkali.
Aboubakar anaongoza orodha ya mfungaji bora, almaarufu golden boot, akiwa amecheka na nyavu mara sita kufikia mechi ya leo.
Maarufu kama Indomitable Lions, Cameroon, watapania kuzoa ushindi mechi ya leo katika pilkapilka za kutwaa kombe la sita la AFCON.
Wamekuwa wafalme wa bara 1984, 1988, 2000, 2002 na 2017.
Nao Firauni wa Misri wanatamani kuondoa kiu ya miaka 10 wanapofukuzia taji la nane baada ya kushinda 1957, 1959, 1986, 1998, 2006, 2008 na 2010.
walianza michuano hii kwa kishindo, walipotoka nyuma na kuibwaga Burkina Faso kwa 2-1 mnamo Januari 9, kabla ya kuandikisha ushindi mkubwa wa 4-1 dhidi ya Ethiopia, siku nne baadaye.
Baadaye walitoka sare 1-1 na Cape Verde kwenye mechi yao ya mwisho ya Kundi A mnamo Januari 17 na kuibuka washindi wa kundi hilo.
Dhidi ya Comoros, vijana hao wa kocha Toni Conceicao waliibuka na ushindi wa 2-1 katika hatua ya 16 bora kutokana na mabao yaliyofungwa na Karl Toko Ekambi na Vincent Aboubakar.
Waliendelea na kupata ushindi wa 2-0 dhidi ya Gambia katika robo-fainali.
Na sasa wenyeji ambao wanatafuta ushindi wa sita wa michuano hii kadhalika watakuwa wakiwania kutinga fainalini kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka mitano.
Mashindano yam waka huu yamekuwa magumu kwa kikosi hicho cha Ma-Pharaoh chini ya kocha Carlos Queiroz ambacho kilianza kampeni kwa kupigwa 1-0 na Nigeria katika mechi ya utangulizi, kabla ya kurejea na kuandikisha ushindi wa 1-0 dhidi ya Guinea Bissau, na baadaye matokeo kama hayo dhidi ya Sudan.
Pointi sita katika mechi tatu ziliwawezesha kufuzu kwa hatua ya maondoano na kukutana na Ivory Coast katika hatua ya 16 bora katika mechi iliyochezwa kwa dakika 120 ambapo Misri walishinda kwa 5-4 kupitia kwa mikwaju ya penalti.