SHAHIDI wa 12 wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, Luteni Denis Urio amemtaka Wakili wa utetezi, Peter Kibatala asimwambie kuwa yuko kizuizini kama hana uthibitisho juu ya hilo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Luteni Urio ametoa kauli hiyo leo Jumanne, tarehe 1 Februari 2022, baada ya Wakili Kibatala kudai amewekwa kizuizini akishinikizwa kuja kutoa ushahidi katika kesi hiyo, inayosikilizwa kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Jiachim Tiganga.
Katika ushahidi wake, Luteni Urio anadai Julai 2020 Mbowe alimuomba amtafutie makomando wa JWTZ, waliofuluzwa au kustaafu jeshini, kwa ajili ya kumsaidia kutekeleza njama za kufanya vitendo vya kigaidi.
Ikiwemo kudhuru viongozi wa Serikali wanaoonekana kikwazo kwa vyama vya upinzani, kuchoma vituo vya mafuta na mikusanyiko ya watu.
Ambapo anadai alimpelekea makomando watatu, Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya, ambao wote ni washtakiwa wenzake Mbowe
Mahojiano kati ya Wakili Kibatala na Luteni Urio yslikuwa kama ifuatavyo;
Kibatala: Ni kweli au si kweli wakati mtoto wako wa mwisho Jackson anazaliwa hukuwa nyumbani, ulikuwa umefichwa na hata mtoto aliletwa akuone ulipokuwa umefichwa, ni kweli au si kweli?
Shahidi: Hili swali nakujibu mara ya pili, siku ya kwanza nilikujibu, kitu cha kwanza unaweza kuwa kizuizini mtu akakueletea familia yako ikuone, inaingia akilini?
Kibatala: Jibu swali langu?
Shahidi: Nataka nikujibu ili usiniulize tena, usifanye kuniulizia swali hilo hilo sawa. Nilikwambia nilimpekea mke wangu kliniki akajifungua nilikujibu hivyo.
Uko kizuzini unaletewa mtoto wako umuone? Hebu fikiri kidogo wewe ni wakili msomi
Kibatala: Ni kweli ama si kweli hata mama yako mzazi ilibidi aje akuone ukiwa kizuizini?
Shahidi: Narudie tena kujibu sijawahi kuwa kizuizini, niko kazini. Narudia tena ukiwa kizuizini unaletewa familia yako kuja kukuona?
Kibatala: Na ni ushahidi wako hata unapokuja mahakamani kutoa ushahidi hakuna maafisa wanaokusindikiza wakiwa na silaha, hilo nalo unalipinga?
Shahidi: Cha kwanza neno kizuizini uliondoe other wise uthibitishe , siko kizuizini nakuja na mawakili wangu mahakamani bila maaskari kunisindikiza
Awali, Wakili Kibatala alidai, Ling’wenya na Kasekwa wanasema Luteni Urio alikamatwa na Jeshi la Polisi kati ya tarehe 8 na 9, ambapo shahidi huyo alikana madai hayo kama ifuatavyo;
Kibatala: Maana yake ni kwamba katika ushahidi wako haujazungumza lolote kusema kwamba sijawahi kukamatwa na maafisa polisi akiwemo Jumanne Malangahe ?
Shahidi: Jumanne ndio nani huyo?
Kibatala: Katika ushahidi wako mkuu haujawahi kutoa ushahidi wa kusema kwamba mimi sijawahi kakamatwa na maafisa Polisi Jumane na Goodluck?
Shahidi: Nitasemaje wakati sijakamatwa si hadi nikamatwe ndio niseme? Nikikamatwa ndio nitasema siwezi kutoa taarifa ambayo haijanitokea mimi.
Tarehe 8 au 9 Agosti 2020 sijawahi kufikishwa kituo cha polisi au mahali popote na wala sijahojiwa mahali popote
Kibatala: Haujamwambia jaji?
Shahidi: Sijamwambia jaji
Kibatala: Maana yake katika ushahidi wako haukuwahi kumwambia jaji mimi sijawahi kufikishwa katika kituo cha Polisi Mbweni tarehe 9 na nikakaa ?
Shahidi: Sijawahi kufikishwa kituo chochote cha polisi wala kuhojiwa na polisi mahali popote, sijawahi kutuhumiwa hayo unayoongea nasikia kutoka kwako.
Kibatala: Wewe una ugomvi na Ling’wenya au Adam?
Shahidi: Sijawahi kugombana nao.
Kibatala: Unaweza kutusaidia kwa nini hawa watu wawili ambao mliishi nao vizuri mpaka watunge uongo zikiwemo kukuona wewe kituo cha polisi Mbweni na Tazara?
Shahidi: Sijawahi kuwa Mbweni, sijawahi kufika Tazara.
Kibatala: Unaweza kutusaidia kwa nini watunge uongo?
Shahidi: Labda wewe uwaulize kwa nini wanatunga uongo wa namna, hiyo lakini mimi sifahamu
Kibatala: Kuhusiana na details za mahabusu wewe uliwekwa Mbweni, Adam anasema ulianza wewe kuwekwa chumba cha mahabusu cha kwake kilifuata?
Shahidi: Narudia tena sijawahi kufika Kituo cha Polisi Mbweni, kwa nini unaniwekea maneno mdomoni mwangu? Kwa nini uniambie kitu ambacho hakipo?
Kibatala: Usikasirike.
Shahidi: Sijakasirika nakwambia kitu fact
Kibatala: Washtakiwa wanasema mshtakiwa wa 1, 2 na 3 wanasema kwamba baada ya wao kukamatwa na kuteswa na Jeshi la Polisi wamehojiwa ni nani aliyewaunganisha na Mbowe? Wao wakakutaja wewe ndio maana ukakamatwa tarehe 8 Agosti 2020.
Ukapewa mateso yakapelekea wewe kutoa ushahidi wako?
Shahidi: Haijawahi kutokea, narudia tena jana uliuliza tarehe 6 ulikuwa wapi nikakwambia nilikuwa kazini.
Shahidi huyo anaendelea kuulizwa maswali ya dodoso na Wakili Kibatala