Maamuzi Kesi ya Mbowe Ijumaa Hii




NI siku 6 mfululizo za uchovu, hasira, vicheko na afya kutokuwa imara kwa shahidi wa 13 kutoka upande wa Jamhuri, askari wa Jeshi la Polisi Tumaini Swila katika kesi namba 16/2021 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu; Halfan Hassan Bwire, Mohamed Lin’gwenya na Adam Kasekwa.

Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ambapo hatimaye leo shahidi huyo amemaliza kutoa ushahidi wake na kudai kuwa alitembelea vituo vya mafuta kadhaa baada ya kupata taarifa kuwa miongoni mwa mambo ambayo inadaiwa kuwa washtakiwa hao walipanga kufanya ni pamoja na kuchoma moto vituo vya mafuta.

Shahidi huyo ameeleza hayo wakati akiulizwa maswali ya dodoso kutoka upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala aliyemuuliza shahidi kuwa alimsikia akisema alitembelea vituo vya mafuta kadhaa na shahidi akadai kuwa ni sahihi.

Wakili Kibatala akamuuliza shahidi kuwa ni sahihi katika ushahidi wake alidai vituo vya mafuta vililengwa kufanyiwa vitu fulani? Shahidi akadai ni sahihi, Kibatala akamuuliza tena shahidi kuwa alitembelea vituo vingapi vya mafuta mbali na Morocco? Shahidi akadai kuwa alitembelea Kituo cha GBP Kilwa Road, PUMA Kilwa Road, BIG BON Kariakoo na PUMA Sinza.


 
Aidha, Wakili Kibatala akamuuliza shahidi kama alimwambia jaji kuwa Kituo cha Morroco kipo Plot namba ngapi na shahidi akadai kuwa alishaeleza kuwa kipo katika barabara na hakueleza kipo plot namba ngapi, wakili akaendelea kumuuliza shahidi kama alimwambia jaji kuwa mmiliki wa kituo hicho ni nani ambapo alimjibu kuwa kuwa hakueleza.

Pia Wakili Kibatala akamuuliza shahidi kama alimwambia jaji kuwa vituo hivyo alitembelea tarehe ngapi na saa ngapi na shahidi akadai kuwa alimwambia jaji kwa kutaja tarehe. Wakili akamuuliza kama alitembelea vituo vyote kwa siku moja ambapo shahidi amedai kuwa ni kweli alitembelea siku moja vituo vyote ambayo ilikuwa ni Agosti 14, 2020, Wakili Kibatala akamuuliza shahidi kama alitaja muda na shahidi akadai kwamba hakutaja.

Kibatala akamuuliza shahidi kama alimwambia jaji alienda na nani siku hiyo wakati anatembelea vituo na shahidi akadai hakueleza.


Aidha Wakili Kibatala akamuuliza shahidi kama atakuwa na tatizo lolote endapo maelezo yake yatapokelewa kama kielelezo mahakamani hapo na shahidi akadai kuwa hakuna tatizo na baada ya jibu hilo la shahidi, Wakili wa Serikali Robert Kidando akamwambia jaji kuwa wao kama mawakili wa serikali hawana pingamizi.

Hatimaye jaji anayesikiliza kesi hiyo, Joackim Tiganga akaeleza kuwa mahakama inapokea maelezo ya Inspector Tumaini Swila ambaye ni shahidi wa 13 kama Kielelezo Namba D5 na baada ya kauli hiyo ya jaji, mawakili wa pande zote mbili wakakubaliana na uamuzi wa jaji.

Wakili wa Utetezi Kibatala akaendelea kumhoji shahidi kama anakumbuka siku ambayo watuhumiwa wanafikishwa mahakamani, walisema upelelezi haujakamilika? Shahidi akadai kuwa ni sahihi, Kibatala akamuuliza shahidi kuwa katika ushahidi wake alisema aliwapeleka watuhumiwa Kisutu na shahidi akadai ni kweli, Kibatala akamuuliza shahidi kama Mbowe alikuwa chini ya uangalizi kabla ya kukamatwa na shahidi akakubali.

Aidha, Kibatala akaendelea kumuuliza shahidi kuwa ni kazi ipi binafsi aliyopewa Halfani Bwire katika kulipua vituo vya mafuta na shahidi akadai kuwa alikuwa na kidaftari chenye michoro ya vituo vya mafuta na akadai kuwa alitaka kulipua vituo vyote, Kibatala akaendelea kumuuliza shahidi kuwa ameyatoa wapi maelezo hayo na shahidi akadai kuwa ameyatoa katika maelezo ya watuhumiwa wote na baada ya hapo Wakili Kibatala akamwambia shahidi asome maelezo ya mshtakiwa Adamu Kasekwa anaposema kuwa Bwire alipewa jukumu la kulipua vituo vya mafuta.


 
Baada ya kupekua na kusoma, wakili akamwambia shahidi aieleze mahakama kuwa mshtakiwa Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya wao walipewa jukumu gani na shahidi akadai kuwa katika maelezo yao hawajaeleza hayo.

Pia Wakili Kibatala akaendelea kumuuliza shahidi kama alithibitisha kuwa tarehe 27 Julai, 2020 walienda kumpokea Tundu Lissu, shahidi akadai kuwa ni sahihi kwa mujibu wa maelezo yao, Kibataka akamuuliza shahidi kuwa yeye akiwa kama mpelelezi ni sahihi alikuwa na washtakiwa saba ambapo shahidi alikubali.

Kibatala akaendelea kumuuliza shahidi kama kuna mshtakiwa yeyote amehukumiwa kifungo katika kesi hiyo na shahidi akadai hakuna aliyehukumiwa.

Baada ya upande wa utetezi kumaliza kumhoji shahidi, sasa ikawa ni fursa ya upande wa jamhuri kwa kumuuliza shahidi maswali ya kufafanua yaliyodumu kwa saa moja na hatimaye Wakili  Kidando akaiambia mahakama kuwa kwa upande wao wamefunga ushahidi hivyo washtakiwa wanapaswa kujitetea ndipo mawakili wa upande wa utetezi walipopinga jambo hilo la watuhumiwa kujitetea wakidai kuwa kwa upande wao wanaona kesi ifutwe kwa madai ya kuwa ushahidi wa mashahidi wote 13 haujajitosheleza hali iliyozua mvutano wa kisheria baina ya pande zote mbili.


Kufuatia hoja hiyo, jaji anayeiongoza kesi hiyo, Joackim Tiganga akaiomba mahakama apewe siku mbili za kupitia mwenendo wa kesi na baada ya hapo Februari 18, 2022 atakuja kutoa maamuzi madogo kama washtakiwa hao wana kesi ya kujibu na baada ya hapo jaji akaahirisha kesi hiyo na washtakiwa wamerudishwa rumande.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad