Mabaharia meli ya Burundi iliyozama waokolewa Tanzania
MELI ya mizigo ya Mv Mbayamwezi ya nchini Burundi iliyokuwa na mabaharia 12, mmoja Mtanzania imezama katika Ziwa Tanganyika eneo la Kata ya Kabwe wilayani Nkasi katika Mkoa wa Rukwa na mabaharia wote kuolewa.
Inaelezwa meli hiyo yenye uwezo wa kubeba shehena ya mzigo wenye uzito wa tani 1,800 ilizama baada ya kupigwa na dhoruba kali na mabaharia hao wakiwa wamevaa maboya waliweza kuelea ziwani kwa zaidi ya saa 12 kabla ya kuokolewa.
Meli hiyo yenye namba za usajili BY 0074 inayomilikiwa na Kampuni ya Red Marine ya nchini Burundi ilikuwa ikitokea katika Bandari ya Mpulungu nchini Zambia ikielekea Burundi, ikiwa imebeba shehena ya malighafi ya kutengenezea saruji yenye uzito wa tani 1,700.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, William Mwamphagale alisema mabahari wote 12 waliokolewa na askari wa majini walioshirikiana na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wavuvi.
Alisema kati ya mabaharia hao, mmoja ni Mtanzania huku wengine sita wakiwa ni raia wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Warundi watano.
Alisema meli hiyo ilipigwa na dhoruba kali Februari 17 mwaka huu saa 5:00 asubuhi. Iliondoka bandari ya Mpulungu nchini Zambia Februari 16.
Mabaharia hao walikimbizwa na kulazwa katika Kituo cha Afya Kirando kilichoko mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi kwa matibabu.
"Jitihada zinafanyika kuwarejesha mabaharia hao nchini Burundi baada ya afya zao kuimarika,” alisema.
Kapteni wa meli hiyo, Ramadhani Morris alisema wakati meli hiyo ikizama ziwani alikuwa wa kwanza kujitosa ziwani.
"Nilipiga mbizi ziwani nilipoibuka nikaanza kupiga mayowe ya kuomba msaada ndipo wavuvi na wengineo walijitokeza kutoa msaada na kutuokoa," alieleza.
Alisema meli hiyo yenye uwezo wa kubeba shehena ya tani 1,800 siku hiyo ya tukio ilibeba tani 1,700.
"Uzito ulikua sahihi bali ni upepo mkali uliiyumbisha meli na kusababisha kuzama ziwani," alisisitiza.
Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Kirando, Dk Benedict Tilamasi alisema mabaharia 11 wametibiwa na kuruhusiwa.
"Tulipowapokea wengi wao walikuwa mahututi lakini baada ya kutibiwa afya zao zimeimarika," alisema.