Madeni ya NSSF, NHIF yashtusha, BUNGE limeitaka serikali kuweka mkakati madhubuti wa kulipa



BUNGE limeitaka serikali kuweka mkakati madhubuti wa kulipa madeni kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, huku likipongeza kupungua kwa deni la Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, aliwasilisha hoja hiyo bungeni jijini Dodoma mwishoni mwa wiki aliposoma taarifa ya mwaka 2020/21.

Alisema walibaini kuwapo kwa madeni ya mifuko kwa serikali na taasisi zake kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.
Kaboyoka alisema kuwa hadi Juni 30, 2020 deni la serikali lilikuwa Sh. trilioni 1.174, kwa kuanzia takwimu za mwaka 2007.

Mwenyekiti huyo alisema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unaidai serikali zaidi ya Sh. bilioni 209.7.

"Madeni haya pamoja na kupunguza ufanisi wa mifuko husika, pia yanaharibu taarifa za mizania ya fedha kinyume cha Kanuni za Kimataifa za Uandaaji wa Hesabu," alitahadharisha.


Kaboyoka alibainisha kwamba madeni hayo yamesababisha mifuko kushindwa kutimiza majukumu yake kisheria kwa ufanisi na kwa wakati.

Alisema deni la PSSSF lililohakikiwa ni Sh. bilioni 731 na walibaini kuwa hadi Juni 30, 2021 serikali ililipa Sh. bilioni 500, mwaka huu ikitoa hati fungani maalumu isiyo taslimu yenye thamani ya zaidi ya Sh. trilioni 1.176.

"Bunge linapendekeza kwamba serikali iendelee na hatua za kulipa madeni husika kwa kutumia njia mbalimbali kama ilivyoanza katika mfuko wa PSSSF. Hatua hizi za serikali ziendelee katika mifuko ya NSSF na NHIF," Kaboyoka alihitimisha.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad