Maelfu ya magari ya kifahari aina Porsche na Volkswagen yameachwa kwenye meli ya mizigo baada ya kushika moto katika Bahari ya Atlantiki ikielekea Marekani.
Meli hiyo iliyopewa jina la Felicity Ace, ilikuwa ikisafiri kutoka Emden nchini Ujerumani kabla ya kushika moto kwenye ufuo wa visiwa vya Azores nchini Ureno.
Gazeti la Ujerumani la Handelsblatt liliripoti kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba magari 3,965, ambayo pia ni pamoja na Audi, Lamborghini na idadi ndogo ya Bentley.
Wafanyakazi wa meli hiyo wameokolewa.
Jeshi la wanamaji la Ureno lilisema hakuna mtu aliyejeruhiwa na moto huo uliozuka siku ya Jumatano, na wafanyakazi 22 walipelekwa hotelini baada ya jeshi la wanamaji, meli nne za wafanyabiashara zinazosafiri katika eneo hilo na Jeshi la Wanahewa la Ureno kukamilisha uokoaji
"Mmiliki wa meli Felicity Ace anawasiliana na wakala husika ili kuandaa mpango wa kuivuta meli," jeshi la wanamaji lilisema katika taarifa.
"Hadi sasa, hakuna chanzo cha uchafuzi wa mazingira kilichorekodiwa."
Kwa mujibu wa Handelsblatt, barua pepe ya ndani kutoka Volkswagen Marekani ilisema kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba magari 3,965 ya VW, Porsche, Audi na Lamborghini.
Volkswagen haikuthibitisha idadi ya magari kwenye meli hiyo, lakini Porsche ilisema ilikuwa na takriban modeli zake 1,100 kwenye meli hiyo.
Kampuni hiyo ilisema "inafahamu tukio lililohusisha meli ya mizigo ya watu wengine inayosafirisha magari ya Volkswagen Group katika Bahari ya Atlantiki".
Bentley alithibitisha kuwa magari yake 189 pia yalikuwa kwenye meli hiyo.
"Tunafanya kazi na kampuni ya usafirishaji ili kupata habari zaidi," msemaji alisema.
Meli hiyo ilikuwa ikisafiri kuelekea kiwanda cha Volkswagen huko Davisville, Rhode Island, kulingana na tovuti ya Marine Traffic.
Mteja mmoja alisema katika Twitter kuwa Porsche yake ilikuwa kwenye meli iliyotelekezwa.