Magereza wafafanua mfungwa, mahabusu kupigwa risasi



​​​​​​​JESHI la Magereza limetoa ufafanuzi kuhusu mfungwa na mahabusu kupigwa risasi mkoani Mtwara.

Kwenye toleo la Nipashe jana, katika ukurasa huu, kulikuwa na habari yenye kichwa cha habari 'Mfungwa, mahabusu wauawa kwa kupigwa risasi wakijaribu kutoroka', ikibainisha kuwa mfungwa aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka 30 gerezani na mahabusu aliyekuwa na tuhuma za mauaji, walifariki dunia kwa kupigwa risasi na askari wa Jeshi la Magereza wakati wakijaribu kutoroka kwenye Gereza Kuu la Lilungu mkoani Mtwara.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Desemba 17 mwaka jana majira ya saa sita mchana likimhusisha mfungwa mwenye namba 321/2021 Juma Mohamed Mwanya na mahabusu Dionis Robat mwenye namba za mahabusu 469/2020, aliyekuwa ameshtakiwa kwa kosa la mauaji katika Mahakama ya Wilaya ya Lindi.

Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi Raymond Mwampashe, aliiambia Nipashe jana kuwa kilichotokea si mauaji, bali wawili hao walifariki dunia wakati wakipelekwa hospitalini baada ya kupigwa risasi walipokaidi kutii amri ya askari wa jeshi hilo.

Alifafanua kuwa askari walilazimika kuwadhibiti kwa kutumia silaha wawili hao baada ya kuwa wamekaidi amri iliyotolewa ikiambatana na kufyatua risasi angani baada ya kumshambulia kwa kitu kizito usoni askari Bamila Maneno.


 
Katika ufafanuzi wake kwa Nipashe juzi kuhusiana na tukio hilo, Mwampashe alisema: "Kwa taarifa nilizoletewa, walifanikiwa kuruka ukuta wa ngome ya magereza muda huo wa mchana na askari wetu waliposhtuka wakapiga filimbi kwa ajili ya kuwazingira lakini walishatoka nje ya gereza na kukimbilia kwenye mashamba ya korosho, hivyo jitihada za kuwatafuta zilianza mara moja kwa askari kuzunguka kila eneo huku wawili wakienda na pikipiki kuzuia barabara kuu," alidai.

Aliongeza kuwa wakati msako ukiendelea askari magereza waliokuwa na pikipiki walikutana na askari wa usalama barabarani na walipowauliza kama wamewaona wafungwa wakipita katika eneo hilo, wakawaambia wameona watu wawili wamepita wakiwa wanakimbia baada ya kuvuka barabara ya kuelekea Newala.

Alidai kuwa baada ya taarifa hiyo, askari walizunguka msitu uliokuwa karibu na eneo waliloelekezwa na wakati msako ukiendelea mwenzao mmoja alipigwa na kitu kizito na mmoja wa waliotoroka huku wakimfuata askari mwenye silaha ili kumpokonya.


Mwampashe aliongeza kuwa hata walipoambiwa wajisalimishe walikataa na wakawa wanazidi kuwakabili askari ndipo walipopigwa risasi kisha wakachukuliwa kwa ajili ya kuwahishwa Hospitali ya Ligula baada ya taratibu za kipolisi katika eneo hilo kukamilika, lakini walifariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.

Kwa mujibu Mwampashe, mahabusu alikuwa na kesi ya tuhuma za mauaji katika Wilaya ya Lindi na alihamishiwa Gereza Kuu la Lilungu Oktoba 9 mwaka jana akiwa anatumikia kifungo cha miaka miwili baada ya kujaribu kutoroka wakati akisubiri kesi yake ya mauaji iendelee huko Lindi.

Alisema mfungwa Mwanya aliyejaribu kutoroka alikuwa kwenye kifungo cha miaka 30 gerezani baada ya kuhukumiwa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa Julai 26  mwaka jana kutumikia adhabu hiyo alipokutwa na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

“Huyu Mfungwa mwili wake tuliwakabidhi ndugu zake lakini mahabusu alizikwa na manispaa baada ya jitihada za kutafuta ndugu zake huko mikoa ya kanda ya ziwa kushindikana," alidai.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad